Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Nchini Jenerali Jacob John Mkunda amekabidhiwa Rasmi Hospitali ya Daraja la Nne ya viwango vya Umoja wa Mataifa iliyojengwa kwa Ushirikiano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Shirikisho la Ujerumani leo tarehe 03 Aprili 2025 Msalato Jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Jenerali Mkunda ameishukuru Serikali ya Shirikisho la Ujerumani kupitia Jeshi la Nchi hiyo kwa namna linavyoshirikiana na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania katika nyanja mbalimbali kama vile Mafunzo, Mazoezi pamoja na Ujenzi wa Miundombinu mbalimbali ikiwemo Hospitali za JWTZ kama vile Hospitali kuu ya Jeshi Lugalo, Chuo cha Tiba cha Kijeshi na Hospitali ya Jeshi ya Kanda ya Arusha.
Aidha Jenerali Mkunda amewataka Madaktari na wauguzi watakaokuwa wakitoa huduma katika Hospitali hii kuitunza ili iendelee kutoa huduma bora kwa kizazi cha sasa na cha baadae kwani miundombinu iliyowekwa katika Hospitali hiyo ni bora na ya gharama kubwa
Naye Balozi wa Shirikisho la Ujerumani hapa Tanzania Mheshimiwa Thomas Terstegen wakati wa makabidhiano ya Hospitali hiyo,ameusifu ushirikiano mkubwa uliopo Kati ya Ujerumani na Tanzania ambapo nchi hizo zimekuwa na ushirikiano wa kindugu ambapo miradi mingi ya maendeleo imetekelezwa kwa ufanisi mkubwa.
Hospitali hiyo imejengwa katika eneo la Msalato Jijini Dodoma ambapo inatarijwa kutoa huduma za tiba kwa Maafisa, Askari na familia zao, Watumishi wa Umma pamoja na wananchi wa Dodoma na maeneo ya jirani.
Sambamba na makabidhiano ya hospitali,Serikali ya Shirikisho la Ujerumani imekakabidhi gari la kubebea wagonjwa aina ya Toyota Land Cruiser kwaajili ya matumizi ya hospitali hiyo.