Watanzania wa tabaka mbalimbali wametakiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki Tamasha la Kuombea Uchaguzi Mkuu, ambalo linalenga kuhimiza amani na mshikamano kuelekea uchaguzi wa mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 2, Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotion, Alex Msama, amesema maandalizi ya tamasha hilo yanaendelea vizuri, na litaanza rasmi jijini Dar es Salaam kabla ya kuendelea katika mikoa mingine 25 nchini.
“Tamasha hili litakuwa la bure ili kuhakikisha kila Mtanzania anaweza kushiriki katika maombi ya kuliombea taifa letu. Tumewashirikisha wachungaji, maaskofu kutoka mikoa mbalimbali ili kuhakikisha tunaiombea nchi amani wakati wa uchaguzi,” amesema Msama.
Ameongeza kuwa tamasha hilo litatangazwa rasmi hivi karibuni, likihusisha waimbaji wa nyimbo za injili kutoka ndani na nje ya nchi, ambao watahamasisha mshikamano wa kitaifa kupitia nyimbo na maombi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Makanisa ya Pentekoste Mkoa wa Dar es Salaam, Mchungaji Emmanuel Mwasoto, amesema tamasha hilo litakuwa jukwaa la madhehebu yote kuungana kuiombea nchi, viongozi wake na wananchi ili uchaguzi upite kwa amani na utulivu.
“Tunawahimiza waumini wote kushiriki kikamilifu katika maombi haya, kwa kuwa uchaguzi ni kipindi nyeti kinachohitaji mshikamano wa kitaifa. Taifa letu linahitaji maombi ili kuhakikisha tunavuka kipindi hiki kwa amani,” amesema Mwasoto.
Ameonya kuwa chaguzi mara nyingine huweza kusababisha migawanyiko iwapo wananchi hawatakuwa wazalendo na kuliombea taifa lao. Hivyo, amesisitiza umuhimu wa kushiriki katika tamasha hilo kwa ajili ya ustawi wa nchi.
Tamasha la Kuombea Uchaguzi Mkuu linatarajiwa kuwa na ushiriki mkubwa wa viongozi wa dini, waumini wa madhehebu mbalimbali na wananchi kwa ujumla, likiwa na lengo la kuhamasisha amani na umoja wa kitaifa.