. Reubeni Lumbagala
Katika haya maisha, binafsi yangu nimeamua kujifunza kwa yeyote bila kujali dini, itikadi ya kisiasa, kabila, umri, jinsi ili mradi analo funzo la kunisaidia. Ndiyo, nimeamua hivyo kwani nimegundua kujifunza ni suala endelevu na kila siku kunahitajika kujifunza mambo mapya kutoka kwa watu mbalimbali.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, ni moja ya walimu wazuri wa falsafa za maisha na siasa, na binafsi nimejifunza mengi kutoka kwake na naendelea kujifunza. Mara kadhaa nimeandika makala kumuhusu yeye kutokana na hotuba nzuri anazozitoa kwa viongozi na wananchi kwa ujumla.
Moja ya hotuba yake nzuri aliyoitoa hivi karibuni ni ile yenye kichwa cha habari “Watu Ni Walewale.” Ndugu msomaji wangu, kama umeisikiliza vyema hotuba hiyo, basi utakuwa umeelimika vya kutosha, lakini funzo kubwa ni kuhusu kuheshimu na kuthamini watu kwani katika maisha tunahitajiana ili kukamilishana, na kufanya maisha yaende vizuri.
Kimsingi, hakuna mtu anayeweza kujitosheleza yeye mwenyewe kwa kila kitu. Hayupo. Kila mtu anahitaji watu wengine nje ya yeye mwenyewe. Hata bilionea namba moja duniani, anahitajit watu wa chini wa kuweza kumzalishia ili aendelee kuwa tajiri. Hata kiongozi wa kisiasa, anahitaji wananchi wa chini wengine wenye hali duni kabisa kiuchumi ili kuweza kumpigia kura, hatimaye aendelee kuongoza katika nafasi mbalimbali za uongozi.
Katika hotuba yake hiyo, Dk. Biteko alisema “Ukiona watu wote tulioko hapa ni walewale, sema ni walewale. Uliyekaa nae hapo pembeni yako ni yuleyule, mtagombana leo lakini ni yuleyule, unawahitaji watu wakati wote. Uwe na cheo usiwe na cheo unawahitaji watu. Kwenye maisha, Mungu ametutengenezea mazingira ya kuwategemea wengine. Hata ulipougua ulihitaji daktari mwingine wa kukutibu wewe, na hata siku ukifa hutajizika, utazikwa na wengine, unawahitaji watu.”
Maneno haya ni mazito sana na yanahitaji unyenyekevu mkubwa kutambua umuhimu wa watu wengine. Hii inatokana na ukweli kuwa wapo baadhi ya watu kutokana na mali na vyeo walivyonavyo wamesahau nguvu ya watu wengine katika kuwafanikisha mambo yao. Mara nyingine wanadhani fedha na mamlaka zao zinawatosha. Kila mtu anahitaji watu wengine.
Wachungaji makanisani, Mashekhe misikitini wanawahitaji watu (washirika/waumini), kukamilisha mahubiri yao katika nyumba za ibada. Mwalimu anahitaji wanafunzi darasani, mfanyabiashara anawahitaji wateja, mwanasiasa anawahitaji wapigakura, daktari anawahitaji wagonjwa, na wengine kadha wa kadha, tunahitajiana. Ndugu yangu, wewe ni nani udharau watu wengine?
Katika haya maisha, hebu tuheshimiane na kuthaminiane. Tusidharauliane kwa misingi ya hali za kiuchumi au vyeo tulivyonavyo. Unayemdharau, unayemuona hafai, hana umuhimu katika maisha yako leo, anaweza kukufaa kesho. Tuishi vizuri, tupendane, kwani hata Mungu anasisitiza upendo miongoni mwetu.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Funguni iliyoko wilaya ya Pangani mkoani Tanga.
Maoni: 0620 800 462.