📌 Serikali kupitia TPDC imetenga Shilingi Bilioni 5.3 kwa ajili ya mradi huu
📌 Gesi asilia ni rafiki wa mazingira, nafuu na salama
📌 Wananchi wa Kata ya Mnazi Mmoja, Lindi wapewa elimu kuupokea mradi
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeendelea kutekeleza kwa vitendo Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia kwa kuanza utekelezaji wa mradi wa usambazaji gesi asilia majumbani katika eneo la Kata ya Mnazi Mmoja na Mingoyo Mkoani Lindi.
Hayo yamesemwa na Meneja Mradi wa Usambazaji wa Gesi Asilia Majumbani Mha. Tumaini Daniel katika mkutano wa hadhara na wanachi wa mtaa wa Muungano kata ya Mnazi Mmoja mkoani Lindi.
Mha. Tumaini ameeleza kuwa “ serikali kupitia TPDC imeendelea kutenga fedha za usambazaji wa gesi asilia majumbani ambapo kwa mwaka wa fedha 2024/25 kiasi cha shilingi bilioni 5.3 kimetengwa kwa ajili ya usambazaji wa gesi asilia katika mikoa ya Lindi (Mnazi Mmoja) na Pwani (Mkuranga).
Aidha,kwa upande wa hatua ya utekelezaji wa mradi, Mha. Tumaini amebainisha kuwa hadi sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 38.18 na mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2025.
‘‘Mradi huu ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati safi ya kupikia (2024-2034) na unahusisha ujenzi wa mtandao wa usambazaji wa gesi asilia kwa nyumba 980 (Nyumba 529 za Mkuranga – Pwani na nyumba 451 Mnazi Mmoja – Lindi). Mtandao wa bomba utakuwa na urefu wa kilomita 47.86, ukiwa ni kilomita 22.9 mkoani Lindi na 24.96 mkoani Pwani’’.
Kuhusu unafuu wa gharama za gesi asilia ya kupikia, Mha. Tumaini alitoa wito kwa wananchi kuitumia gesi hii ipasavyo pindi mradi utakapo kamilika kwani nishati ya gesi asilia ni gharama nafuu, rafiki wa mazingira, inaokoa muda na inapatikana wakati wote hivyo basi kwa faida hizo serikali haitegemei kuona wananchi wakiendelea na matumizi ya kuni na mkaa ambazo zinachangia katika uharibifu wa mazingira na uchafuzi wa hali ya hewa.
Akiongea na wananchi wa mnazi mmoja, Afisa Maendeleo ya Jamii Bw. Oscar Mwakasege ameeleza kuwa, pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali, TPDC itaendelea kushirikisha wananchi katika utekelezaji wa shughuli zake kupitia majukwaa mbalimbali ya elimu kama mikutano ya hadhara, vyombo vya habari, makongamano, warsha pamoja na michezo.
‘‘Tangu kuanza kwa mradi wa usambazaji wa gesi asilia majumbani kata ya mnazi mmoja , TPDC imekua ikishirikisha wananchi kupitia mikutano ya hadhara, elimu kupitia vyombo vya habari na elimu ya nyumba kwa nyumba ili kujenga uelewa wa mradi kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama wa miundombinu pamoja na kutambua fursa zinazoambatana na mradi kama vile ajira. Zoezi la utoaji elimu ni endelevu na kila hatua ya mradi wananchi hushirikishwa’’. Ameeleza Oscar.

Kwa upande wake, Diwani wa kata ya mnazi mmoja Mhe. Said Mohammed Mchinjita aliishukuru TPDC kwa kuendelea kusambaza gesi asilia mnazi mmoja pamoja na kuwajibika kwenye shughuli za maendeleo ikiwemo kutoa fedha za ujenzi wa ofisi ya serikali ya Mtaa wa Ruaha-Kata ya mnazi mmoja.
Aidha, Diwani alitoa rai kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa wataalamu pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama wa mali na vifaa vya wakandarasi ili mradi huu ukamilike kwa wakati.
Aidha, wananchi wameendelea kuipongeza TPDC kwa kuchochea soko la ajira ambapo kupitia miradi yake wananchi wamekua wakinufaika na fursa za ajira ambazo zimewapa kipato cha kuendesha maisha yao.
Bi. Hawa Fumau Dadi mkazi wa Mtaa wa Mnazi mmoja ambaye ni mnufaika wa ajira kwenye mradi wa gesi majumbani ameishukuru TPDC kwa kutekeleza mradi huu kwani umetoa fursa za ajira za muda mfupi ambazo zinawasaidia wananchi kupata fedha za kukidhi mahitaji ya kila siku.
‘‘Nashukuru kwa kupata kazi katika mradi huu wa TPDC katika mtaa wa Muungano mnazi mmoja, tunashukuru tumepata ajira inayotuwezesha kupata fedha za kuendesha maisha ya kila siku, hivyo wananchi tusilale tukae tayari na kuweka mazingira wezeshi ya kuupokea mradi kama kuwa na jengo la jiko’’ alisema Bi.Hawa.
Serikali kupitia TPDC itaendelea na jukumu la kuhakikisha wananchi wanapata nishati safi ya kupikia kwa kutenga fungu la fedha kwenye bajeti yake ya maendeleo ya kila mwaka.
TPDC TUNAWEZESHA