……………….
TANGA – Wumini wa dini ya Kiislam na Watanzania kwa ujumla wametakiwa kuyaishi yale waliyojifunza ndani ya Mwezi mtukufu wa Ramadhan ikiwa ni pamoja kujenga tabia ya kuwa na hofu ya Mungu.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Rajabu Abdulrahman wakati akitoa salamu zake kuelekea Sikuku ya Iddi el Fitri ambayo inatarajiwa kuswaliwa Machi 31 mwaka huu sawa na Mwezi Mosi Shaawal mwaka 1446.
Aidha Rajab Abdulrahmana amewapongeza wafanyabiashara wa Mkoa wa Tanga kwa kuuheshimisha mwezi wa Ramadhan kwa kutopandisha bei za bidhaa zao tofauti na miaka mingine .
“Niwapongeze sana wafanyabiashara wa Mkoa wa tanga bei za bidhaa ukiangalia kwa upatikanaji wake kabla ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na ndani ya Mwezi mtukufu wa Ramadhani bei ni zile zile kwa hiyo tunawashukuru na tunawapongeza na tunapokwenda kuimaliza ibada hii ya mwezi mtukufu wa Ramadhani nipende kuwaasa sana wana Tanga wenzangu tuendelee kuishi kwa namna ambavyo Mwenyezi mungu (S.W) ametuamrisha, tuache yale yote Mwenyezi Mungu ametukataza na hiyo maana halisi ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani” amesema Rajabu Abdulrahman.
Katika hatua nyingini mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa amewataka wakazi wa Mkoa Tanga kuendelea kudumisha amani, upendo,Umoja na Mshikamano huku akionya wale wale wote wenye nia ovu ya kupanga ama kujaribu kuleta vurugu ndani mkoa wa Tanga.
“Tusikubali waje watu waturubuni kwa maneno ya kisiasa, waje watu waturubuni kwa nama wanavyojua wao wenyewe kwa waliowatuma kuvunja amani ndani ya mkoa wetu wa Tanga,Tumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Rais amejipambanua wazi katika suala zima la amani wenye kuichezea amani hana msalie Mtume kwa sabababu tunajua madhara yake ” amesema Mwenyekiti wa ccm Mkoa wa Tanga Rajab Abdul Rahman.
Mbali na hayo Rajab Abdulrahman amewataka wakazi wa Mkoa wa Tanga kuendelea kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa na afya njema ili aweze kuwatumikia Watanzania.