Na Ashrack Miraji – Fullshangwe Media
Watu saba wamefariki dunia na wengine 75 wamejeruhiwa katika ajali mbili tofauti zilizotokea wilayani Same.
Ajali ya kwanza ilitokea majira ya saa saba usiku wa kuamkia leo katika eneo la Njoro, ikihusisha basi la Kampuni ya Osaka lililokuwa likielekea Dar es Salaam. Ajali hiyo ilisababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi watu 52.
Ajali ya pili ilihusisha basi aina ya Costa la Kampuni ya Mkokota, iliyotokea majira ya saa mbili asubuhi leo katika kona za milima ya Ilamba. Basi hilo lilipinduka, na kusababisha vifo vya watu sita na majeruhi 23. Waliofariki dunia walikuwa wanakwaya waliokuwa wakisafiri kutoka Chome kuelekea Ndolwa.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Same, Dkt. Alex Alexander, amesema kuwa majeruhi wa ajali ya kwanza walipokelewa hospitalini majira ya saa nane usiku, huku majeruhi wengine 23 pamoja na miili ya marehemu sita wakifikishwa hospitalini mchana wa leo.
Baadhi ya majeruhi wa ajali ya kwanza wameeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo kilikuwa mwendokasi, hali iliyosababisha dereva kushindwa kulimudu gari. Chanzo cha ajali ya pili kimeelezwa kuwa ni hitilafu ya mfumo wa usukani (steering rod).
Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, ameonesha masikitiko yake kutokana na vifo hivyo na kuwasihi madereva kuwa waangalifu wanapopita wilayani Same, hasa kutokana na hali ya hewa yenye upepo mkali. Aidha, amewataka abiria kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapobaini hali yoyote inayoweza kuhatarisha usalama wao wakiwa safarini, ikiwemo mwendokasi.