Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa, kimechangia jumla ya Sh 1,553,500 kwa ajili ya matibabu ya Katibu Mwenezi wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) Taifa, Sigrada Mligo, anayehitaji huduma ya afya katika Hospitali ya Peramiho.
Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM Taifa, anayeshughulikia Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makalla, alipitisha harambee hiyo leo wakati wa mkutano wake na wananchi katika Uwanja wa Mashujaa, Wilaya ya Mufindi, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tatu katika mikoa ya Mbeya na Iringa.
Awali, Makalla alisema kuwa akiwa mkoani Mbeya jana, alitoa pole kwa Sigrada na kuagiza chama chake katika mkoa wa Njombe kumtembelea na kumpa salamu za faraja. Pia alizungumza naye kwa simu na kufahamu kuwa anahitaji msaada wa matibabu ili apate nafuu na kurejea katika hali yake ya kawaida.
“Sigrada anahitaji msaada wa matibabu, na mimi kama mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi natoa wito kwa wenezi wenzangu tushirikiane. Nimechangia, lakini bado tunapaswa kuendelea kumsaidia ili apate huduma inayostahili,” alisema Makalla.
Katika harambee hiyo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Iringa, Asas Abri, alichangia Sh milioni moja, huku kiasi cha Sh 553,500 kikipatikana kutoka kwa wanachama wa CCM Wilaya ya Mufindi.