*Dodoma*
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, ameagiza Miradi Mikubwa na ya Kati ya madini ambayo tayari imekwishapewa leseni kuanza utekelezaji wake mara moja ili kuchochea ukuaji wa sekta na kuleta manufaa kwa taifa kwa ujumla na kutimiza azma ya Serikali kutoa leseni hizo.
Amesema hayo, leo Machi 28, 2025 Jijini Dodoma wakati akizungumza katika Mkutano maalum na Chemba ya Migodi Tanzania (TCM) kwa lengo kujadili masuala mbalimbali yanayohusu Sekta ya Madini ili kuboresha uendelezaji na usimamizi wa shughuli za uchimbaji na biashara ya madini kwa manufaa ya sekta na taifa kwa ujumla, ikiwa ni sehemu ya ratiba yake ya kukutana na makundi yote yayojihusisha na mnyororo mzima wa Sekta ya Madini nchini.
Waziri Mavunde amesema Serikali inataka kuhakikisha kuwa Miradi yote ya Uchimbaji Madini iliyopangwa kuanza inaanza mara moja bila kucheleweshwa, na kuwa Serikali kwa upande wake imejitahidi kurahisisha taratibu kwa wawekezaji na sasa ni wakati wa Sekta binafsi kuchukua hatua kwa upande wao.
“Serikali imefanya kazi yake, tumeondoa vikwazo vingi na kurahisisha utaratibu. Sasa ni jukumu la wawekezaji kuhakikisha kuwa miradi inaanza kutekelezwa mara moja” amesema Waziri Mavunde.
Aidha, Waziri Mavunde ameahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa madini, ikiwemo TCM, katika kutatua changamoto zinazowakabili wawekezaji ili kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kukua kwa kasi na kufikia lengo la uchangiaji wake katika Pato la Taifa (GDP) na maendeleo ya kiuchumi kwa ujumla.
“Sisi kama Serikali tutakaa pamoja na taasisi husika ili kuangalia changamoto zilizopo na kuzitatua kwa haraka. Hatutaki ukiritimba wowote ambao unaweza kuchelewesha maendeleo ya Sekta hii muhimu, Serikali hii ni moja na ina lengo moja” amesisitiza Mavunde.
Kwa upande mwingine, Waziri Mavunde amesisitiza umuhimu wa utafiti katika Sekta ya Madini, akieleza kuwa maendeleo endelevu yanategemea uwekezaji mkubwa katika tafiti zinazosaidia kuongeza uzalishaji na tija. Aidha, amepongeza juhudi za wadau wa sekta hiyo katika kutekeleza Maono ya Vision 2030; Madini ni Maisha na Utajiri inayotekelezwa na Wizara kwa lengo la kuongeza maeneo yaliyofanyiwa utafiti wa kina, kuongeza ajira kwa Watanzania, Miradi ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR), na uwezeshaji wa Watanzania kupitia Ushirikishwaji wa Watanzania (Local Content).
Kuhusu mchango wa Sekta ya Madini kwenye uchumi wa taifa, Waziri Mavunde ameeleza kuwa Sekta hiyo imeendelea kukua kwa kasi, ambapo mwaka 2022/23 ilichangia asilimia 7.2 ya Pato la Taifa, huku mwaka 2023/24 mchango wake ukifikia asilimia 9.0. Serikali inalenga Sekta hiyo ichangie angalau asilimia 10 ifikapo mwaka 2025, kama ilivyoainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2025.
Katika ukusanyaji wa Maduhuli ya Serikali, Waziri Mavunde amesema mapato yameongezeka maradufu, ambapo mwaka wa fedha wa 2015/16 yalikuwa shilingi bilioni 162, lakini kufikia mwaka wa fedha 2023/24 yaliongezeka hadi shilingi bilioni 753 ambapo kwa mwaka huu wa fedha wa 2024/25, Serikali inalenga kukusanya shilingi trilioni 1, lengo ambalo linaonekana litafikiwa kulingana na mwenendo wa ukusanyaji mapato.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Chemba ya Migodi Tanzania (TCM) Mhandisi Benjamin Mchwampaka ameiongeza Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kuendelea kuwashirikisha katika hatua mbalimbali za majadiliano kwa lengo la kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji nchini.
Amesema kuwa, Tanzania ni moja ya nchi chache ambazo Sekta Binafsi inapewa nafasi ya kushiriki vikao muhimu sambamba na Maafisa wa Serikali akitolea mfano ushiriki wa pamoja wa Wizara na TCM katika mikutano mikubwa kama Mining Indaba ambayo hufanya Afrika Kusini kila mwaka.