FARIDA MANGUBE, MOROGORO
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeeleza kuwa itaendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara badala ya kutumia nguvu kama vile kufunga maduka kwa wale ambao hawajalipa kodi kwa wakati.
Akizungumza wakati akitoa elimua kwa mlipa kodi kupitia moja ya redio mjini Morogoro, Meneja Msaidizi wa Huduma kwa Mlipakodi wa TRA, Chacha Boaz Gotora, alisema kuwa mamlaka hiyo imejipanga kuhakikisha wafanyabiashara wanapata uelewa mzuri kuhusu sheria za kodi ili kuepusha usumbufu katika biashara zao.
“Tunatilia mkazo utoaji wa elimu kwa walipa kodi ili kuwawezesha kuelewa wajibu wao. Ni muhimu wafanyabiashara kufahamu kwamba kulipa kodi ni jukumu la kila mmoja kwa maendeleo ya taifa,” alisema Gotora.
Akifafanua kuhusu mifumo ya kodi, Gotora alieleza kuwa kodi ya mapato kwa wafanyakazi inatozwa kulingana na kiwango cha mshahara.
Mfano wake ni kwamba mfanyakazi anayepokea mshahara wa kuanzia shilingi 200,000 anapaswa kulipa kodi kwa mujibu wa viwango vilivyowekwa na TRA.
Kwa upande wa wafanyabiashara, Gotora alisema kuwa wanagawanyika katika makundi tofauti, ikiwa ni walipakodi binafsi na makampuni. Kila kundi lina taratibu zake za ulipaji kodi, ambapo wafanyabiashara wadogo na wa kati wanatakiwa kujikadiria kodi zao kulingana na mtaji walio nao.
“Ikiwa mfanyabiashara ana mtaji wa shilingi milioni 100, anatakiwa kuzingatia viwango vya kodi vilivyowekwa na TRA,” alieleza.
Kwa mujibu wa TRA, mfanyabiashara yeyote mwenye mauzo ya shilingi 700,000 anatakiwa kulipa kodi ya shilingi 250,000 kwa mwaka, huku makampuni yakitakiwa kulipa kodi kulingana na faida wanayopata baada ya gharama za uendeshaji.
Aidha ameendelea kusisitiza kuwa wafanyabiashara na wafanyakazi wanapaswa kuelewa na kuzingatia sheria za kodi ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na kutofuata taratibu sahihi za ulipaji kodi.