FARIDA MANGUBEM MOROGORO
Zaidi ya vitongoji 16,000 vinatarajiwa kupata umeme ndani ya miaka miwili ijayo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha tatizo la ukosefu wa nishati hiyo linabaki kuwa historia.
Haya yanakuja licha ya kwamba tayari Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umekamilisha mradi maalumu wa kusambaza umeme kwenye migodi ya madini, ambapo zaidi ya maeneo 550 yamepatiwa huduma hiyo.
Vilevile, REA imepeleka umeme wa uhakika kwenye vituo 553 vya kusambazia maji safi na salama kwa wananchi kote nchini.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa REA Mhandisi Hassan Saidy, ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa wakala huo, wakati wa ufunguzi wa kikao cha sita cha baraza hilo.
Mhandisi Saidy amesema kuwa REA ni taasisi yenye uwezo mkubwa wa kutekeleza na kufanikisha malengo ya serikali kwa manufaa ya taifa. Amebainisha kuwa wakala huo umeendelea kutekeleza miradi mikubwa yenye matokeo chanya kwa Watanzania.
Hadi sasa, REA imefanikisha miradi minne mikubwa, ikiwemo mradi wa kupeleka umeme vijijini awamu ya tatu, ambapo vijiji 5,259 vimepatiwa umeme. Mradi mwingine mkubwa uliofanikishwa ni ule uliohudumia mikoa minane, ambapo maeneo 426 yamenufaika na nishati hiyo.
Aidha, Mhandisi Saidy amesema kuwa miradi mingine inayoendelea kutekelezwa ni pamoja na:
Mradi wa Ujazilizi Awamu ya Pili B, ambapo vitongoji zaidi ya 1,600 vitapatiwa umeme.
Mradi wa Ujazilizi Awamu ya Pili C, utakaonufaisha vitongoji 1,800.
Mradi wa umeme kwa Wilaya ya Lindi, ambapo vitongoji 293 vitapatiwa nishati hiyo.
Mradi Maalumu wa Kila Jimbo, unaolenga kupeleka umeme kwenye vitongoji 15 kwa kila jimbo, sawa na jumla ya vitongoji 3,060 kote nchini.
“Kazi hizi zote zinatekelezwa kwa weledi na ufanisi mkubwa na wafanyakazi wa REA, hivyo kuna kila sababu ya kuwapongeza kwa juhudi zao chini ya mwavuli wa serikali yetu inayoongozwa na mama shupavu,” alisema Mhandisi Saidy.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Nishati, Bibi Ziana Mlawa, amewataka wajumbe wa baraza hilo kutumia kikao hicho kujadili masuala yenye tija ili kusaidia taasisi kufikia malengo ya serikali ya kusambaza huduma ya umeme kwa wananchi.
Naye, Mwakilishi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) Taifa, Dkt. Elias Mtungilwa, amesema kuwa wajibu mkubwa wa chama hicho ni kusimamia na kulinda haki na maslahi ya wafanyakazi, huku pia wakihakikisha kuwa haki hizo zinapatikana na kulindwa ipasavyo.
Baraza la Wafanyakazi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), likiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhandisi Hassan Saidy, limekutana mjini Morogoro kwa muda wa siku mbili kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya taasisi hiyo.