Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kumekuwa na ongezeko la ufanisi katika matumizi ya rasilimali za Serikali katika miaka ya hivi karibuni hali inayoashiria Serikali imefanikiwa kukuza uwazi, uwajibikaji na kuendelea kukuza utawala bora.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Shirika Nyanga imesema Rais Dkt. Samia amesema hayo leo wakati wa hafla ya kupokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2023-2024 pamoja na Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) iliyofanyika Ikulu.
Rais Dkt. Samia amesema pamoja na mapungufu yaliyotajwa ambapo hata hivyo mengi ni ya miaka mingi, lakini kumekuwa na ongezeko la ufanisi wa matumizi ya rasilimali za Serikali.
“Niipongeze timu nzima ya CAG kwa kazi waliyoifanya wamekagua hesabu za fedha, lakini wamekagua ufanisi wa miradi na Taasisi mbalimbali. Wamefanya uchunguzi na kaguzi za mifumo ya TEHAMA kama zinafaya kazi inayotakiwa. Ukaguzi uliofanywa unatupa taswira ya matokeo ya hatua zinazochukuliwa na Serikali kupitia taasisi za umma” amesema Rais Dkt. Samia.
Aidha, Rais Dkt. Samia ameshukuru jitihada zinazofanywa na Taasisi za umma na kuzitaka zitumie vizuri rasilimali za Serikali na kufuata taratibu zinazotakiwa za matumizi ya rasilimali hizo.
Wakati huo huo, Rais Dkt. Samia amepongeza kazi kubwa iliyofanywa na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Crispin Francis Chalamila ambapo amebainisha kuwa Taarifa imeonyesha kuongezeka kwa ufanisi ndani ya TAKUKURU.
Rais Dkt. Samia amesema Taarifa imeonyesha kukuza ufanisi ndani ya Taasisi zetu za umma, lakini imeinyayua Tanzania kutoka nafasi iliyokuwepo kwenye mapambano dhidi ya rushwa pamoja na kukuza kiwango cha ufahamu na kujenga ujasiri kwa Watanzania kwa ujumla, kufahamu maana ya rushwa.
Rais Dkt. Samia amesisitiza umuhimu wa kujenga uelewa wa mapambano dhidi ya rushwa kwa vijana kuanzia shule ya msingi mpaka vyuo vikuu.
Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Dkt. Samia ameweka wazi kuwa Serikali ipo tayari kuendelea kufanyia kazi maoni na mapendekezo yaliyotolewa ndani ya taarifa hizo mbili, kwa nia ya kujenga utawala bora ndani ya nchi.
Tukio la leo ni la kikatiba kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 143 (4), ambapo inamtaka CAG kuwasilisha taarifa ya ukaguzi wa hesabu za Serikali kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.