Mbunge wa Rombo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amewafuturisha wakazi wa wilaya ya Rombo na kusisitiza umuhimu wa kudumisha umoja na mshikamano ulioachwa na waasisi wa Taifa pamoja na kuzingatia falsafa ya 4R za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hafla hiyo, iliyofanyika Jumatano, Machi 26, 2025, wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro, iliongozwa na Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Shaabani Mlewa ambapo Prof. Mkenda alieleza kuwa mkusanyiko huo haukuwa tu kwa sababu ya chakula, bali ulidhihirisha upendo, mshikamano, na umoja uliopo Rombo na Tanzania kwa ujumla.
Sheikh Mlewa alimpongeza Prof. Mkenda kwa uzalendo wake wa kipekee kwa wana Rombo, akimtaja kama kiongozi anayejali maendeleo ya jimbo lake huku akiwataka viongozi wa dini, taasisi, na wananchi kumwombea Prof. Mkenda ili aendelee kutekeleza majukumu yake ya kitaifa na kibunge kwa ufanisi.
Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala, alisifu ushirikiano kubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayosukumwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani imekuwa rahisi kwake kutekeleza majukumu ya kiutendaji.
Hafla hiyo iliwakutanisha makundi mbalimbali, yakiwemo watu wenye ulemavu, bodaboda, taasisi za dini na serikali, wakuu wa idara, vyama vya siasa, na watoto.