****
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeishauri TEMESA kuhakikisha inaongeza kasi ya kusimamia mkandarasi anaetekeleza mradi wa ujenzi wa kivuko kipya cha Mafia Nyamisati ili umalizike haraka na wananchi waweze kupata huduma ya kivuko.
Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya mradi huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Naghenjwa Kaboyoka amesema wananchi wa maeneo ya Mafia na Nyamisati wanahitaji huduma ya kivuko na Serikali ipo inatazama kwa ukaribu kuona mradi huo unakamilika kwa wakati.
“kwahiyo tunasema kwamba hili jambo litupiwe macho tuone kwamba huu ujenzi wa kivuko hiki kipya cha Mafia na Nyamisati unafanywa kwa ukamilifu ili wananchi wapate ile huduma iliyotakiwa, hivyo tunawashauri na tunawataka mjiongeze, mjiongeze kwa kiasi kikubwa kukamilisha mradi huo.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Japhet Hasunga ameiomba Serikali kuhakikisha fedha zinatolewa kwa wakati ili mradi huo uweze kukamilika kwa wakati huku akiitaka TEMESA kuhakikisha inasimamia maendeleo ya mradi huo kila siku kwa kuwepo katika eneo la ujenzi.
“TEMESA mnatakiwa kuwepo eneo la mradi kila siku kusimamia utekelezaji wa huu mradi, mnatakiwa kuusimamia kuwa sehemu ya huu mradi, muiunde timu haraka iwezekanavyo iweze kuunusuru huu mradi, iwepo pale na itoe taarifa kila siku kwamba tumefikia hapa tumenasa wapi nini kimefanyika, vifaa hivi vimekuja hii imefungwa hii haijafungwa. Amesisitiza Mhe. Hasunga.
Akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa kivuko hiko kipya, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Lazaro Kilahala amesema kivuko kipya kinachojengwa kitakuwa na uwezo wa kubeba tani 120, abiria 300 na magari madogo 10.
Ameongeza kuwa kivuko hicho kitakuwa na uwezo zaidi kulinganisha na kinachoendelea kutoa huduma hivi sasa cha MV. KILINDONI ambacho kinao uwezo wa kubeba abiria 200 pekee.
Kilahala amesema kuwa ujenzi wa kivuko hicho kipya kitakachokuwa kinatoa huduma kati ya Mafia na Nyamisati unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Agosti mwaka huu.