Na Ashrack Miraji Fullshagwe Media
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamisi Mwinyijuma ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Muheza, Mkoani Tanga, amegawa hati 33 za mashamba ya Kwabada, katika shamba la Lewa, ambalo lilikuwa na mgogoro wa ardhi wa muda mrefu. Mgogoro huo umekuwa ukiendelea kwa takribani miaka 9 na leo umepatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Akizungumza wakati wa hafla ya ugawaji wa hati hizo, Mhe. Mwinyijuma alitoa shukrani za dhati kwa ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Kamishna wa Aridhi Mkoa wa Tanga, na kampuni ya Urasimishaji na Upimaji wa Ardhi, Ardhisol, kwa juhudi kubwa walizofanya kuhakikisha wananchi wa Kata ya Kwabada wanapewa hati zao.
“Mimi binafsi, nitowe shukrani zangu za dhati kwa ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza na kampuni ya Ardhisol kwa kazi kubwa ambayo wameifanya. Leo hii wananchi wa Kata ya Kwabada wanakabidhiwa hati zao, na binafsi nimejiskia faraja kubwa sana. Hii itapunguza migogoro ya ardhi kwa asilimia kubwa katika wilaya yetu ya Muheza, sambamba na Mkoa wetu wa Tanga,” alisema Mhe. Mwinyijuma.
Aidha, aliendelea kusema: “Hata hivyo, nisingependa kusikia matatizo ya ardhi yanaendelea hapa jimboni kwetu. Kesi nyingi ambazo zinaweza kumalizika haraka, hazipaswi kuwa na migogoro zaidi. Ni muhimu kumaliza migogoro ya ardhi haraka ili wananchi waweze kupata utulivu.”
Alisisitiza kwa wananchi kuwa hati wanazopata ni mali na kwamba ziweze kutumika vizuri ili kuongeza uzalishaji wa mazao. “Hati hizi ni mali, na kwa hivyo ni muhimu kuzitunza na kuzitumia kwa kuongeza uzalishaji wa mazao yetu,” alisema.
Pia, Mhe. Mwinyijuma aliwakumbusha viongozi wa Halmashauri ya Muheza kuwa utatuzi wa migogoro ya ardhi ni kipaumbele chake na kwamba atazidi kushirikiana na ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri kutatua changamoto zinazohusiana na ardhi katika wilaya hiyo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Dkt. Jumaah Mhina, alieleza: “Kile kinachofanyika hapa leo ni kuondoa wasiwasi na upotoshaji. Serikali imeamua kwa dhati kuhakikisha kuwa wananchi wanapata hati zao, na hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha kwamba maeneo haya yanatumika kwa maendeleo.”
Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Ardhisol, Kelvin Lyamuya, alieleza changamoto walizokutana nazo wakati wa zoezi hilo, akisema: “Hii ilikuwa kazi kubwa lakini kwa ushirikiano na ofisi ya Halmashauri ya Muheza na Kamishna Mkuu wa Aridhi Mkoa wa Tanga, zoezi hili limefanikiwa. Ingawa kulikuwa na changamoto za kijografia na upotoshaji wa taarifa, tumefanikiwa kuwawezesha wananchi kupata hati zao.”
Mmoja wa wananchi waliokabidhiwa hati, Festo Kidumba, alisema: “Hii haikuwa kazi rahisi, lakini tumefanikisha. Tunashukuru kwa timu nzima ya Ardhisol na Halmashauri ya Wilaya ya Muheza kwa kufanikisha zoezi hili.”
Wananchi hao walipongeza juhudi za serikali kupitia Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhamasisha na kutekeleza mchakato wa urasimishaji wa ardhi. “Leo hii, wananchi tumekabidhiwa hati zetu, na tunashukuru kwa serikali yetu inayotutambua na kutusimamia kwa dhati,” alisema Kidumba