Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2023/24 kutoka Bw. Charles Kichere kwenye hafla fupi iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 27 Machi, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdory Mpango na Viongozi mbalimbali mbalimbali wakiwa kwenye hafla ya kupokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2023-2024 pamoja na Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ikulu Jijini Dar es Salaam
………..
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, amewasilisha ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2023/2024, akibainisha kuwa hadi Juni 30, 2024, deni la Taifa limefikia Shilingi trilioni 97.35. Hii ni ongezeko la Shilingi trilioni 15.1 kutoka trilioni 82.25 iliyoripotiwa mwaka wa fedha uliopita.
Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan leo Machi 27, 2025, CAG Kichere amesisitiza kuwa ongezeko hilo linajumuisha deni la ndani la Shilingi trilioni 31.95 na deni la nje la Shilingi trilioni 65.4. Pamoja na ukuaji wa deni, tathmini inaonyesha kuwa bado lipo katika kiwango himilivu kulingana na viwango vya kimataifa.
Kwa mujibu wa CAG, viashiria vikuu vya tathmini vinaonyesha kuwa thamani halisi ya deni la nje ni asilimia 23.6 ya Pato la Taifa, chini ya ukomo wa asilimia 40. Aidha, deni la jumla ni asilimia 41.1 ya Pato la Taifa, likiwa ndani ya ukomo wa asilimia 55. Malipo ya deni kwa kutumia mapato ya nje yamefikia asilimia 127.5, chini ya ukomo wa asilimia 180, huku malipo ya deni kwa kutumia mapato ya ndani yakiwa asilimia 14.5, chini ya ukomo wa asilimia 18.
CAG Kichere amepongeza hatua ya Serikali katika kufuatilia na kutekeleza mapendekezo yanayotolewa na ofisi yake kupitia ripoti za ukaguzi. Amemshukuru Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Moses Kusiluka, kwa kuratibu vyema utekelezaji wa mapendekezo hayo kupitia makatibu wakuu wa wizara mbalimbali.
“Katika ripoti za nyuma, nilitoa mapendekezo kadhaa kuhusu usimamizi wa rasilimali za umma na ukusanyaji wa mapato. Nimeona juhudi za Serikali katika kufanyia kazi mapendekezo haya, hasa kupitia miongozo inayotolewa na Ofisi ya Rais,” amesema Kichere.
Katika ripoti yake, CAG ameeleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024, jumla ya hati 1,301 zilitolewa, ikiwa ni ongezeko la hati 92 kutoka hati 1,209 zilizotolewa mwaka wa fedha uliopita. Kati ya hizo, hati 220 zinahusu Tamisemi, 218 mashirika ya umma, 513 Serikali Kuu, 19 vyama vya siasa, na 332 miradi ya maendeleo.
Katika tathmini ya ubora wa hati hizo, asilimia 99.5 (hati 1,295) zilikuwa safi, asilimia 0.4 (hati 5) zenye shaka, na asilimia 0.1 (hati 1) ilikuwa mbaya. CAG amesema matokeo haya yanaonyesha kuwa utayarishaji wa hesabu za Serikali umeendelea kuimarika na unazingatia viwango vya kimataifa vya uandaaji wa hesabu.
Pamoja na ongezeko la deni la Taifa, ripoti ya CAG inaashiria uimara wa usimamizi wa fedha za umma, huku Serikali ikiendelea kutekeleza mapendekezo ya ukaguzi ili kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali za nchi