Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam, Tanzania – Kikosi cha Simba SC kinatarajiwa kuondoka nchini alfajiri ya Machi 28 kuelekea Misri kwa kutumia ndege ya Egypt Air, kwa ajili ya mchezo wao dhidi ya Al Masry kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kwa mujibu wa Msemaji wa klabu hiyo, Ahmed Ally, wachezaji waliokuwa sehemu ya timu ya taifa, Taifa Stars, wataungana na wenzao nchini Misri ili kukamilisha maandalizi ya mchezo huo. Aidha, nyota wa kikosi hicho, Camara na Mukwala, tayari wamewasili na kuungana na wenzao kwa maandalizi zaidi kabla ya safari.
Ahmed Ally amesisitiza kuwa maandalizi yanaendelea kwa umakini mkubwa, huku akiwataka mashabiki wa klabu hiyo kuwa na imani na timu yao licha ya changamoto zinazoweza kujitokeza.
> “Kila Mwanasimba atambue kwamba pamoja na mipango tuliyonayo lakini lazima tujipange, lazima tujiandae na hasa kama timu yenyewe inatokea Misri. Ukiangalia michuano ya Afrika ilivyo utaona kwamba Misri ndio nchi iliyoingiza timu nne kwenye robo fainali,” alisema Ahmed Ally.
Aliongeza kuwa Simba SC inatambua ugumu wa mechi dhidi ya Al Masry, lakini dhamira yao kuu ni kufuzu hadi hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.
Kuhusu suala la Uwanja wa Benjamin Mkapa, msemaji huyo alieleza kuwa ukaguzi wa uwanja huo tayari umeshafanyika na matokeo rasmi yanatarajiwa kutolewa hivi karibuni.
“Bado majibu hayajatoka, lakini katika mazungumzo wanasema kuna maboresho makubwa kwenye uwanja ukilinganisha na mara ya mwisho walipofanya ukaguzi, hivyo kuna nafasi kubwa ya kucheza kwenye uwanja huo,” alieleza.
Simba SC inajiandaa kwa mtihani mgumu dhidi ya Al Masry, huku mashabiki wakisubiri kwa hamu kuona timu yao ikipambana kusonga mbele katika michuano hiyo ya kimataifa.