Na Prisca Libaga, Arusha
MAPATO ya mradi wa Nyumba 90 za makazi zilizopo eneo la Olorieni jijini Arusha zinazomilikiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Umma (PSSSF) yamepanda hadi kufikia wastani wa Sh.bilioni 1.6 kwa mwaka.
Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, AbdulRazaq Badru alisema hayo jana mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) iliyotembelea mradi huo na kuridhishwa na uwekezaji uliofanyika.
“Tangu mwaka 2013 mradi huu umeendelea kuvuna faida na fedha zote zilizotumika kujenga mradi huu ambazo ni shilingi bilioni 13.91 zilikuwa
zimesharejeshwa hadi kufikia mwaka 2012,” alisema.
Alisema mradi huo wenye nyumba 90 za makazi ofisi 26, shule ya chekechea na sehemu za burudani unawapangaji asilimia 91 na nyumba hizo zimekuwa kimbilio la wafanyakazi wa Taasisi nyingi za kimataifa zenye makao mkauu jijini Arusha.
“Uwekezaji wa mradi huu umefanyika kwa kuzingatia miongozo mbalimbali ikiwemo; muongozo wa uwekezaji wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii unaotolewa na Benki Kuu ya Tanzania na sera ya uwekezaji ya Mfuko na mpango wa uwekezaji wa mwaka,”alisema
Kwa mujibu wa Badru,Kutokana na nyumba hizo kujengwa mwala 1996 na kukamilika mwaka 1998 wameamua kufanya ukarabati wa nyumba 23 kwa gharama za TZS Bilioni 2.5 na ukarabati huo utakamilika Juni mwaka huu.
“Upangaji kwa sasa ni asilimia 91 kutokana na ukarabati wa nyumba 23 ambapo wapangaji waliokuwa kwenye nyumba hizo wamepatiwa sehemu ya kukaa na zikikamilika Juni mwaka huu watarejea na upangaji utakuwa asilimia mia moja,”alisema.
Aidha alisema licha ya mafanikio hayo wanakabiliwa na deni la Sh.milioni 750 linalotokana na wapangaji wa zamani katika nyumba hizo na wanaendelea na utaratibu wa kutumia madalali wa mahakama kukusanya fedha hizo.
Alisema PSSSF inaendelea na majukumu yake kikamilifu ikiwemo kusimamia mitaji,kukusanya michango pamoja na kulipa mafao na mishahara ya watumishi kwa wakati.
Mwenyekiti wa Kamati ya PIC, Agustine Vuma alisema wajumbe wameridhishwa na mradi huo wa kuigwa ambao unaleta faida,kukuza uchumi na umeongeza thamani na mandhari ya Jiji la Arusha, kutokana na utunzaji mzuri wa mazingira na usafi.
“Tunaupongeza uongozi wa PSSSF kwa kazi kubwa na nzuri ya uwekezaji,ukusanyaji wa michango na kulipa mafao kwa wakati lakini tunashauri muweke mipango ya ukarabati wa muda mrefu na mfupi, pamoja na kuweka mikakati madhubuti ya kukusanya madeni kwa sababu hii siyo huduma ni biashara,”alisema.









