Dk. Reubeni Lumbagala
Miaka minne ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani imetimia kikamilifu. Katika kipindi hiki cha miaka minne, mengi ya maendeleo yamefanyika katika kila wizara, idara na vitengo. Kiufupi, hakuna sehemu ambayo haijaguswa kwa namna ya kimaendeleo. Hakuna, narudia tena hakuna ambako hakujaguswa kimaendeleo. Maendeleo yameonekana ambapo tunaweza kusema miaka minne hii imekuwa ya maziwa na asali. Mambo ni Bam-bam.
Siri ya kufanikiwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inatokana na uwepo wa raslimali fedha iliyokusanywa kama kodi kutoka kwa wananchi. Wananchi kupitia shughuli mbalimbali wanazozifanya za kuwaingizia vipato hulipa kodi serikali, kazi inayoratibiwa vyema na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Hakuna muujiza wowote unaoweza kufanyika wa nchi kupata maendeleo bila kukusanya kodi kutoka kwa wananchi wake, ndiyo maana wahenga walisema “Nchi itajengwa na wananchi wenyewe.”
Tunapoangazia miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan miongoni mwa maeneo ya kujivunia ni pamoja na ongezeko kubwa la makusanyo ya kodi ambapo kwa miaka minne hii, makusanyo ya mapato yameongezeka kwa asilimia 78 yaani kutoka shilingi Trilioni 11.92 hadi Trilioni 21.20.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari Machi 12, 2025 jijini Dodoma, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda alisema ” Wakati Mheshimiwa Rais Samia anaingia madarakani tukifananisha toka mwaka huu wa fedha umeanza Julai 2024 mpaka Februari 2025, miezi nane, ukifananisha na miezi nane kabla haijaingia madarakani Julai 2020 mpaka Februari 2021, Mamlaka ya Mapato ilikusanya shilingi Trilioni 11.92, lakini leo tunazungumzia miezi nane hiyo hiyo, tumeweza kukusanya jumla ya shilingi Trilioni 21.20, hili ni ongezeko la asilimia 78.”
Ikumbukwe, kaulimbiu ya Serikali ya Awamu ya Sita ni “Kazi Iendelee,” lakini kazi ya kuwapatia wananchi maendeleo haiwezi kufanikiwa bila raslimalifedha. Ndiyo maana, mkazo wa Rais Dk. Samia ulikuwa ni kuongeza ukusanyaji wa mapato kwa ustawi wa maendeleo ya wananchi.
UTEKELEZAJI WA MAAGIZO YA RAIS SAMIA WAPAISHA MAPATO
Rais Dk. Samia alitoa maagizo matatu kwa Mamlaka ya Mapato ili kuongeza mapato ambayo ni msingi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi. “Alitoa maagizo matatu makubwa kwa TRA ambayo ni kuhakikisha TRA inakusanya kodi kwa weledi, kupanua wigo wa ukusanyaji kodi kwa kujenga mahusiano bora na walipakodi na kutumia 4R (Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga Upya) na walipakodi,” alisisitiza Kamishna Mkuu Mwenda katika mkutano huo.
Walipakodi nchini wanazo changamoto zao ambazo kama zikifanyiwa kazi ipasavyo, zitasaidia kuongeza mapato na kustawisha shughuli na biashara zao kwa ujumla. Kwa maelekezo ya Rais Dk. Samia, utaratibu wa kusikiliza kero za walipakodi ili ziweze kufanyiwa kazi na manufaa ya pande zote yaani serikali na walipakodi ulianza. “Tumetenga siku nzima ya Alhamisi ya kila wiki kuanzia kwenye wilaya, mikoa na hata kwenye ofisi kuu, Makamishna wa kodi waliopo, Mameneja wa kodi wa mkoa na wilaya. Hii yote ni kuwasililiza lakini kubwa zaidi ni kutatua changamoto walizonazo na wamekuwa wakija wengi na matatizo mengi yametatuliwa,” amesema Kamishna Mkuu Mwenda.
Kimsingi, ni faraja kuona mwamko wa wananchi wa kulipa kodi ambayo ni msingi wa maendeleo umeongezeka sana katika miaka hii minne ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan. Mwamko huu unatoa hakikisho juu ya upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kugharamia shughuli mbalimbali za maendeleo kama vile elimu, afya, maji, umeme, masoko, kilimo, uvuvi, barabara, ufugaji, uwezeshaji wananchi kiuchumi na miradi mingine kadha wa kadha. Kwa hakika, tukiendelea na mwendo huu, kama Taifa tutakuwa na uhakika wa kupiga hatua kubwa za maendeleo maana nyenzo ya fedha itakuwepo.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Funguni ya wilayani Pangani, mkoani Tanga.
Maoni: 0620 800 462