Mkurungenzi wa Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Moshi Kabengwe akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 21, 2025 jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo wakati akitangaza majina ya waombaji kazi ambao wamepita katika mchujo wa kwanza 112,952 kati ya 135,027 waliyoomba nafasi za kazi TRA.
Afisa Mkuu wa Uhusiano kwa Umma Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Rachel Mkunda akiwa katika mkutano na waandishi wa habari.
…….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetangaza majina ya watu 112,952 waliokidhi vigezo vilivyowekwa kwa ajili ya kupata ajira na kuwaita kwenye usaili wa mchujo wa kuandika ili waweze kuwapata watu 1,596 wanaohitajika kuajiriwa na TRA katika kada mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 21, 2925 jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkurungenzi wa Usimamizi wa Rasilimali Watu na utawala wa TRA, Moshi Kabengwe amesema katika mchakato huo Mamlaka imezingatia taratibu zote za kupata waajiriwa kupitia usaili.
Kabengwe amesema kuwa majina ya waliofanikiwa yatatangazwa kwenye tovuti ya TRA (www.tra.go.tz) kuanzia leo machi 22,2025 na pia taarifa zitatumwa moja kwa moja kwa kila muombaji kupitia barua pepe yake aliyotumia wakati wa kuomba kazi, ambapo imeeleza tarehe, mahali na muda wa usaili.
“TRA imepitia kwa umakini mkubwa maombi yote yaliyopokelewa na kupata waomba kazi 112,952 waliokidhi vigezo vilivyowekwa na hivyo kustahili kuitwa kwenye usaili wa mchujo wa kuandika (written interview) ambao unatarajiwa kufanyika kuanzia Machi 29 hadi 30 mwaka huu.” amesema Kabengwe.
Amesema kuwa usaili huo wa mchujo wa kuandika utafanyika katika Mikoa tisa ambayo ni Dar es Salaam ikihusisha Mkoa huu na Pwani, Zanzibar (Unguja na Pemba), Arusha ambayo itahusisha waombaji kutoka Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga.
Mikoa mingine ni Dodoma ambayo itahusisha waombaji kutoka Morogoro, Dodoma, Singida, Iringa na Tabora, Pia mkoa wa Mtwara ambayo itakuwa na watu kutoka Mtwara, Lindi na Ruvuma, huku mkoa wa Mbeya ukihusisha mikoa ya Mbeya, Songwe na Rukwa.
Mkoa wa Mwanza itahusisha, Mwanza, Shinyanga, Mara na Simiyu wakati wakati Kagera ikihusisha Kagera na Geita na Kigoma ambayo itahusisha waombaji kutoka Kigoma na Katavi.
Kabengwe amesema utaratibu maalumu umeandaliwa kwa waombaji kazi wenye mahitaji maalumu ili waweze kufanya usaili huo bila usumbufu.
“Mchakato huu utaendeshwa na mshauri Mtaalamu (Consultant) na Mamlaka itasimamia kwa karibu ili kuhakikisha haki inatendeka kwa waombaji wote, tunatoa wito kwa waombaji kazi wote kujiandaa vyema katika hatua zote za usaili ili kufanya vizuri katika mitihani hiyo na kuepuka udanyanyifu wa aina yeyote,”amesema Kibengwe.
Amesema kuwa waombaji watakaofaulu kwenye usaili wa mchujo wa kuandika wataitwa kwenye usaili wa mahijiano kwa tarehe, siku na mahali watakapotaarifiwa baadaye.