Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amempongeza Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah, Rais wa Jamhuri ya Namibia kwa kuapishwa kwake, na amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuendeleza umoja na mshikamano katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili dunia, kiwemo: mtikisiko wa uchumi, mabadiliko ya tabianchi na kuzorota kwa hali ya usalama.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Sharifa B. Nyanga imesema Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo wakati wa sherehe za uapisho wa Rais wa nchi hiyo.
Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah zilizofanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 35 ya Uhuru wa nchi hiyo ambapo Rais Dkt. Samia alikuwa Mgeni Rasmi.
Katika hotuba yake, Rais Dkt. Samia alisema siku ya leo ni ya kihistoria si tu kwa Namibia bali pia Afrika kwa ujumla kwa kuapishwa Rais wa pili mwanamke barani Afrika.
Akimuelezea Rais Nandi-Ndaitwah, Rais Dkt. Samia amesema bila shaka Namibia imepata kiongozi shupavu, mahiri na mwenye uzoefu mkubwa katika chama na Serikali tangu enzi za harakati za kupigania uhuru ambapo alitumia nafasi yake kupigania usawa wa kijinsia na haki za wanawake duniani.
“Tanzania tunakuita Mama SWAPO jina ulilopewa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, umeipa heshima Afrika na Namibia kwa sababu ushindi wako umekuwa ni fahari kwetu sisi Tanzania kuona binti tuliyemlea na kumkuza kisiasa, na kumuoza amepewa heshima na wananchi kuliongoza taifa. Majirani zako wa Magomeni katika Jiji la Dar es Salaam wanafurahi pamoja nawe siku ya leo.” amesema Rais Dkt. Samia.
Rais Dkt. Samia alieleza kuwa, Tanzania iliamua kwa dhati kupigania usawa wa mataifa mengine hata baada ya kupata uhuru, tuliamini uhuru kwetu haukuwa na maana ikiwa wengine hawako huru. Alisisitiza kuwa Namibia na Tanzania ni ndugu wa damu ingawa tunatenganishwa na mipaka
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia alimshukuru kwa ushirikiano Rais Mstaafu wa Namibia aliyemaliza muda wake, Mhe. Nangolo Mbumba na kumtakia maisha mema ya
kustaafu baada ya kazi kubwa aliyowafanyia wananchi wake.