Na Fullshangwe Media
Katika hafla ya Iftar iliyoandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) mnamo Machi 20, 2025, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, aliwahakikishia wananchi kuwa Benki Kuu itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa uthabiti ili kuimarisha uchumi wa nchi na kulinda ustawi wa wananchi dhidi ya changamoto za soko la dunia.
Akizungumza mbele ya viongozi wa serikali na wa kidini, Gavana Tutuba alieleza kuwa BoT inatekeleza sera madhubuti za kifedha ili kuhakikisha mfumuko wa bei unabaki kwenye viwango vinavyodhibitika, jambo ambalo litapunguza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi.
“Tunajitahidi kuhakikisha uchumi wa Tanzania unakuwa imara na endelevu. Kupitia sera bora za fedha, tunalinda thamani ya shilingi na kupunguza mfumuko wa bei, ili kila mwananchi aweze kuhimili gharama za maisha,” alisema Gavana Tutuba.
Katika hotuba yake, Gavana Tutuba aliwataka wananchi kuwa waangalifu na kujiepusha na mikopo umiza pamoja na upatu, akisisitiza umuhimu wa kutumia huduma za kifedha kutoka kwa taasisi zilizopewa leseni na BoT.
“Wananchi wahakikishe wanapata huduma za kifedha kutoka kwa watoa huduma walioidhinishwa na Benki Kuu. Mikopo umiza na upatu vimekuwa vikisababisha madhara makubwa kwa watu wengi, na tunasisitiza kutumia vikundi vya ushirika na SACCOS zilizopewa leseni rasmi,” aliongeza Tutuba.
Gavana Tutuba pia aliweka bayana kuwa BoT itachukua hatua kali kwa watoa huduma za kifedha wanaokiuka masharti ya leseni zao kwa kuwatoza wananchi gharama zisizo halali au kuendesha shughuli zao kinyume cha sheria.
“Watoa huduma wote wanapaswa kuzingatia masharti ya leseni zao. Tukibaini ukiukwaji wa sheria, Benki Kuu haitasita kuchukua hatua, ikiwemo kufuta leseni na kuwachukulia hatua kali za kisheria,” alionya Gavana Tutuba.
Katika hafla hiyo, Mufti Mkuu wa Tanzania, Shekhe Abubakar Zuber, alisisitiza umuhimu wa kudumisha amani na mshikamano wa kitaifa, akiwataka wananchi kuwa mstari wa mbele katika kuzuia viashiria vyovyote vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa nchi.
“Mwaka huu tunapaswa kuishi kwa kauli mbiu ya ‘Wajibika, Jitambue, Acha Mazoea.’ Tanzania ni mfano wa amani katika Afrika Mashariki, na tunapaswa kuilinda kwa nguvu zetu zote,” alisema Shekhe Zuber.
Hafla hiyo ya Iftar ilihudhuriwa na viongozi wa dini, serikali na sekta ya kifedha, ikiwa ni sehemu ya juhudi za BoT katika kujenga mshikamano na kuimarisha uchumi wa Tanzania kupitia mfumo thabiti wa kifedha.