Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), jana tarehe 19 Machi, 2025 limewafuturisha wadau mbalimbali pamoja na watoto yatima kutoka kituo cha “Lady Fatima Orphanage Centre” kilichopo Kigamboni kwa kuwapatia chakula na mahitaji mengine muhimu kwa ajili ya Mfungo wa Mwezi wa Ramadhani pamoja na sikukuu ya Eid.
Akizungumza katika hafla hiyo, iliyofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee VIP, Sheikh wa mkoa wa Dar es Salaam – Sheikh Walid Alhad Omar ambaye alikua mgeni rasmi, amesema kuwa katika mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani jamii haina budi kuwa na huruma kwa wale wasio na uwezo, ambao ni wajane na yatima ili kuwasaidia waweze kutekeleza ibada ya funga vizuri.
“Katika mwezi wa Ramadhani, tunahimizwa kuwa wakarimu na kuwasaidia watu wasio na uwezo kwani ni sehemu muhimu katika mwezi huu ili nao waweze kufurahia mfungo wa mwezi huu,” alisema Sheikh Walid.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TASAC, Naho. Mussa Mandia ameipongeza Menejimenti ya TASAC kwa kutimiza miongozo ya mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa kuwapatia mahitaji muhimu yatima.
“Nawapongeza Menejimenti kwa kuwagusa yatima wa kituo cha watoto yatima cha Lady Fatima Orphanage Centre cha Kigamboni kwa kuwapatia chakula na mahitaji mengine muhimu ili waweze kufunga mwezi huu vyema na kusherehekea sikukuu ya Eid,” amesema Naho. Mandia.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum amehimiza umoja na mshikamano miongoni mwa wadau na wafanyakazi wa TASAC kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa karibu ili kuongeza ufanisi katika kutoa huduma.
“Kukutana pamoja pia ni fursa nzuri ya kusherehekea mafanikio ya kazi na malengo yaliyofikiwa. Huu ni wakati mzuri wa kutathmini mafanikio yaliyopatikana na kujivunia juhudi za pamoja za wafanyakazi na wadau, huku tukiboresha umoja na mshikamano,” amesema Bw. Salum.