Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo na Waziri wa Mambo ya Nje, Uhamiaji na Wamisri Waishio Nje wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Mheshimiwa Dr. Badr Abdelatty, wameshiriki hafla ya ufunguzi wa kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Misri lililofanyika jijini Dar es Salaam ambapo kwa pamoja wamesisitiza umuhimu wa nchi zao kukuza ushirikiano wa Kibiashara na Uwekezaji, kwa manufaa ya wananchi wake.
Kongamano hilo limeshirikisha wafanyabiashara mbalimbali kutoka Tanzania na Misri, likilenga kuimarisha ushirikiano wa biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.
Akizungumza katika ufunguzi wa Kongamano hilo, Mhe. Balozi Kombo amewakaribisha Wafanyabiashara wa Misri kuwekeza na kufanya biashara nchini kwani Tanzania ni nchi yenye mazingira mazuri ya uwekezaji na vivutio vya kutosha katika sekta mbalimbali.
Aidha ameongeza kuwa utayari mkubwa wa kisiasa uliopo kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dakta Samia Suluhu Hassan na Rais wa Misri Abdel Fatta el-Sisi ni kielelezo tosha cha kuziwezesha nchi hizi kuendelea kupanua wigo wa ushirikiano katika maeneo mengi zaidi yakiwemo maji kupitia miradi ya ujenzi wa mabwawa kama Bwawa la Kufua Umeme wa Maji la Julius Nyerere ambalo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 99.
Mhe. Kombo amewasihi Wafanyabiashara wa Tanzania kutomuangusha, kwa kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo nchini Misri na kuanzisha miradi ya ushirikiano na Wafanyabiashara wa nchi hiyo ili kuunganisha nguvu, kukuza uchumi na kuimarisha Biashara ya Kimataifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje, Uhamiaji na Wamisri Waishio Nje wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Mheshimiwa Dkt. Badr Abdelatty, amewataka Wafanyabiashara wa Tanzania kufungua zaidi milango ya biashara na uwekezaji katika maeneo ya teknolojia, kuanzisha miradi ya ushirikiano katika kilimo, biashara ya mbolea na kuibua fursa za biashara ikiwemo uvuvi, kupitia Bonde la Mto Nile, ili kukuza maendeleo ya watu wake na kupanua soko la ajira kwa vijana.
Ameipongeza Tanzania kwa jitihaha zake katika kuimarisha mazingira ya Uwekezaji na Biashara kwani zimesaidia nchi hizo mbili kuendelea kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na uhusiano wa Kimataifa.
Mhe. Dkt. Abdelatty, yuko nchini kwa ziara ya kikazi ambapo pamoja na mambo mengine, atatembelea yake mradi wa ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere lililoko Rufiji mkoani Pwani.