Na John Bukuku Dar es Salaam
Msemaji wa kundi la Samia 4 By 4 amepongeza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, akieleza kuwa ni hatua kubwa kwa Tanzania kuwa na Rais wa kwanza mwanamke katika historia ya Afrika Mashariki.
Amesema kuwa Rais Samia amekuwa kinara wa maendeleo kupitia dira yake inayojikita katika nguzo nne kuu: ustahimilivu, mageuzi, ujenzi mpya, na maridhiano.
“Katika kuadhimisha miaka minne ya Rais Samia, tunashuhudia harakati kubwa za maendeleo na mshikamano. Uongozi wake umeleta mageuzi makubwa katika utawala na kuinua uchumi wa nchi,” amesema.
Ameongeza kuwa mfumo wa uongozi wa Rais Samia umeimarisha demokrasia, maendeleo ya uchumi, na mshikamano wa kitaifa.
“Ngumu yetu ya 4 By 4 inaonyesha jinsi Rais Samia anavyosonga mbele kuleta maendeleo. Changamoto zipo, lakini kama ilivyo kwa gari la 4 By 4, linapokutana na matope huendelea mbele bila kusimama. Hivyo ndivyo tunavyomuona Rais wetu,” amesema.
Kwa kutambua mafanikio hayo, kundi hilo limetangaza kuandaa msafara mkubwa wa magari 4 By 4 mnamo Aprili 5, mwaka huu, ambapo magari takribani 100 yataanza safari kutoka Dar es Salaam hadi Pangani.
Amesema kuwa safari hiyo itapitia Hifadhi ya Saadani, ambapo msafara utapokelewa Pangani na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso. Lengo la safari hiyo ni kuhamasisha utalii wa ndani na kuonyesha mshikamano wa Watanzania, huku ikichochea biashara na burudani katika maeneo hayo.
“Tutakuwa tukisimama na kusherehekea mafanikio ya miaka minne ya Rais Samia, huku tukisaidia jamii kupitia mradi wa Samia Delivery Kit. Kupitia mradi huu, tutajikita katika kusaidia afya ya mama na mtoto kwa kugawa mahitaji mbalimbali kwa wanawake wajawazito katika maeneo yote tutakayopita,” amesema.
Ametoa wito kwa mashirika ya kibiashara na taasisi mbalimbali kushiriki kikamilifu katika harakati hiyo, ili kuunga mkono dhamira ya Rais Samia ya kuisukuma Tanzania mbele bila kurudi nyuma.
“Hatuadhimishi tu miaka minne tangu Rais Samia kuapishwa, bali pia tunasherehekea urithi wa maendeleo unaoendelea kushamiri kila kona ya nchi yetu. Tunamuunga mkono kiongozi mwenye dira thabiti, anayesimama imara kuhakikisha Tanzania inapiga hatua bila kusimama,” amesema.