Na Silivia Amandius,
Kagera.
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Mhe. Stephen Masato Wasira, anatarajiwa kuanza ziara ya siku tatu mkoani Kagera kuanzia Machi 22 hadi Machi 25, 2025. Lengo la ziara hiyo ni kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, kusikiliza na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa mkoa huo.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Machi 19, 2025 katika ofisi za CCM zilizopo Manispaa ya Bukoba, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Kagera, Hamimu Mahmudu Omary, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kumpokea kiongozi huyo ambaye kwa mara ya kwanza anafanya ziara mkoani humo akiwa na wadhifa wa Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa Hamimu, Mhe. Wasira atapokelewa rasmi Machi 22, 2025 katika Uwanja wa Ndege wa Bukoba kuanzia saa tano hadi saa tano na nusu asubuhi. Baada ya mapokezi, atasaini vitabu vya wageni katika ofisi za chama hicho, kisha saa nane mchana ataelekea Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, kata ya Kemondo, katika ofisi za KCU ambapo atafanya mkutano mkubwa wa hadhara na wananchi wa Halmashauri hiyo pamoja na wananchi wengine wa mkoa wa Kagera.
“Niwaombe wananchi mjitokeze kwa wingi kumpokea kiongozi wetu mkubwa na kushiriki katika mikutano ambayo itatoa fursa ya kuwasilisha changamoto na mapendekezo yao kwa chama na serikali,” amesema Hamimu.
Ameongeza kuwa, Machi 23, 2025, Mhe. Wasira atazuru wilaya ya Karagwe ambapo atakutana na wanachama, wananchi pamoja na viongozi wa CCM kupitia mkutano wa ndani. Aidha, Machi 24, atafanya ziara wilayani Ngara ambapo atakutana pia na wananchi na viongozi kupitia mkutano mwingine wa ndani.
Mhe. Wasira anatarajiwa kuhitimisha ziara yake Machi 25, 2025 mjini Bukoba kwa kufanya kikao cha majumuisho kilicholenga kuimarisha chama, kusalimiana na wanachama pamoja na kupokea maoni kutoka kwa wananchi ili kuimarisha utekelezaji wa Ilani ya CCM mkoani humo.