Na Mwandishi wetu, London.
Baada ya kukamilika kwa kampeni ya kuitangaza Tanzania kupita msafara wa utangazaji utalii ya “My Tanzania Roadshow 2025” katika nchi za Ujerumani, Ubelgiji, Uholanzi na Uingereza, Taasisi zilizoko chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo ni TTB, TANAPA, na NCAA yamefanya majadiliano na Wakala Wauzaji utalii wa Tanzania katika Jiji la London nchini Uingereza.
Kikao hicho kilihusisha wakala 15 wanaouza utaii wa Tanzania nchini Uingereza na kuhudhuriwa na Maafisa Utalii toka Ubalozi wa Tanzania Uingereza na Maafisa waandamizi toka TTB, TANAPA, na NCAA.
Lengo la kikao hicho ni kuongeza ufahamu wa Wakala hao juu ya mwenendo wa utalii nchni Tanzania kwa ujumla husan, mazao mapya ya utalii yanayopatikana nchini na kuwaeleza juhudi za Serikali kuboresha miundombinu ya utalii ndani na nje ya hifadhi.
Akitoa taarifa baada ya majadiliano hayo Mkurugenzi wa Masoko toka TTB, Bw. Ernest Mwamwaja alisema, majadiliano hayo yametoa fursa kwa mashirika ya wizara kubaini mtazamo na mahitaji maalum ya watalii wa soko la Uingereza. Na kwa upande mwingine yamesaidia ujumbe huo wa Wizara kufahamu changamoto wanazopata Wakala wauzaji utalii hao na namna bora ya kuzitatua ili kuendelea kuboresha mazingira rafiki kwa watalii wanaotembelea Tanzania.
Afisa anayehughulikia masuala ya utalii katika ofisi za ubalozi wa Tanzania Uingereza, Bw. Tim Henshall alitoa matokeo ya utafiti aliouanya juu ya mwenendo wa utalii wa Tanzania katika soko la uingereza. Utafiti huo ulibaini, pamoja na mambo mengine, maeneo wanaopenda kupendelea watalii kutoka Uingereza, namna wanavyopata taarifa kuhusu Tanzania, na mtazamo wao juu ya ubora wa vivutio na huduma za utalii.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Biashara toka TANAPA, Bi. Jully Lyimo, aliwasilisha mada juu ya juhudi za TANAPA kuongeza wigo wa mazao ya utalii na kuongeza wigo wa kijiografia wa utalii nchini. Aidha, Afisa Uhifadhi Mwandamizi- utalii toka NCAA, Bw. Iddi Mavura, ametabainisha juhudi za Shirika katika kuboresha miundombinu ya utalii ndani ya hifadhi ya Ngorongoro na kuongeza mazao mapya ya utalii ili kuongeza mtawanyiko wa wageni ndani ya hifadhi.
Ujumbe kutoka Tanzania ulitumia fursa ya kikao na mawakala hao kuwaomba kupigia kura vivutio vya Utalii Tanzania ambavyo vimeinngizwa na mtandao wa World Travel awards (WTA) kuwania tuzo katika vipengele mbalimbali.