Mwenyekiti wa Bodi Maendeleo Bank PLC Profesa Ulingeta Mbamba akizungumza jambo wakati akizindua huduma ya Internet Banking maarufu kama Click Bank Smile katika hafla iliyofanyika leo Machi 18, 2025 jijini Dar es Salaam (PICHA NA NOEL RUKANUGA)
Mwenyekiti wa Bodi Maendeleo Bank PLC Profesa Ulingeta Mbamba (wa kwanza kushoto) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Maendeleo Bank PLC Lomnyaki Saitabau akizindua huduma ya Internet Banking maarufu kama Click Bank Smile katika hafla iliyofanyika leo Machi 18, 2025 jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Maendeleo Bank PLC Lomnyaki Saitabau akizungumza jambo wakati akizindua huduma ya Internet Banking maarufu kama Click Bank Smile katika hafla iliyofanyika leo Machi 18, 2025 jijini Dar es Salaam.
Picha za matukio mbalimbali ya washiriki wakiwa katika hafla ya uzinduzi wa huduma ya Internet Banking maarufu kama Click Bank Smile.
……..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Maendeleo Bank PLC imezindua huduma ya Internet Banking maarufu kwa jina Click Bank Smile ambayo inampa fursa mteja kutumia huduma za benki kwa njia ya mtandaoni katika kufanikisha huduma mbalimbali ikiwemo miamala ya kifedha kwa urahisi pamoja na uwezo wa kusimamia fedha bila kutembelea tawi la benki.
Huduma ya Click Bank Smile inatoa nafasi kwa wateja wa Maendeleo Benki kuhamisha fedha kutoka akaunti moja hadi nyingine, kulipia huduma za bidhaa, kufatilia taarifa za akaunti kwa wakati, kufanya malipo ya mara kwa mara pamoja na kuomba hundi na kadi za ATM.
Akizungumza leo Machi 18, 2025 jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa huduma ya Internet Banking maarufu kama Click Bank Smile, Mwenyekiti wa Bodi Maendeleo Bank PLC Profesa Ulingeta Mbamba, amesema kuwa click bank smile ni jibu sahihi kwa mahitaji ya wateja wa leo wanaotaka huduma za haraka, salama pamoja na kupatikana mahali popote na muda wowote.
Profesa Mbamba amesema kuwa huduma hiyo itaongeza ufanisi wa biashara hasa kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati pamoja na kuokoa muda na gharama za wateja kutokana kila kitu kinapatikana kwa njia ya mtandao.
“Huduma ya internet banking itawanufaisha wateja pamoja na kusaidia ukuaji wa uchumi wa wananchi kwa kuongeza ujumuishi wa kifedha nchini. Hivyo Maendeleo Bank inaimarisha uchumi wa kidigitali na kuhakikisha jamii inapata huduma za kifedha kwa urahisi” amesema Profesa Mbamba.
Profesa Mbamba amefafanua kuwa kwa mujibu wa Fin – Scope Survey ya mwaka 2023 kiwango cha upatikanaji na matumizi ya huduma rasmi za kifedha kiliongezeka kutoka 76% hadi kufikia 89%, huku akieleza kuwa hali hiyo imechangia uimarikaji wa huduma za kifedha kwa njia ya kidigitali kwa njia ya simu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Maendeleo Bank PLC Lomnyaki Saitabau, amesema kuwa huduma ya Click Bank Smile ni miongoni mwa mipango mikakati wa mwaka 2025 ya kuboresha huduma kwa kuanzisha bidhaa bunifu, rafiki na zinazokidhi matakwa ya wateja pamoja na kuimarisha mifumo ya TEHAMA itakayosaidia utoaji huduma kwa haraka.
Saitabau amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa mstari wa mbele kuhimiza matumizi ya teknolojia ili kuboresha sekta mbalimbali ikiwemo fedha, hivyo huduma ya Click Bank Smile ni juhudi za kuhakikisha wateja wanapata huduma za kibenki kwa njia ya kisasa, salama na rafiki kwa mazingira.
“Lengo ni kuhakikisha huduma za fedha zinawafikia wananchi wengi ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara, wakulima, wafanyakazi, wajasiriamali wa sekta zote. Click Bank Smile ni fursa kwa watanzania kutumia huduma za kifedha kwa njia ya kidijitali ili kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara na kuongeza ufanisi wa miamala ya kifedha” amesema Saitabau.
Ametoa wito kwa watanzania kuhusani wateja wa Maendeleo Bank PLC kutumia huduma mpya ya internet Click Bank Smile kuboresha maisha ya kifedha.