Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amewasilisha Ujumbe Maalum wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. Emmerson Mnangagwa katika Ikulu ya Harare.
Katika mazungumzo yao, Mhe. Waziri Kombo amemshukuru Rais Mnangagwa na wananchi wa Zimbabwe kwa mapokezi yao mazuri, huku akimfikishia salamu za upendo na mshikamano kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na vyombo vya habari baada ya kuwasilisha ujumbe huo, Mhe. Kombo ameeleza kuwa lengo la ziara yake lilikuwa ni kumtambulisha rasmi Prof. Mohammed Janabi, Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, kama Mgombea wa SADC kwa nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
Kwa upande wake, Prof. Janabi ameeleza kuwa, endapo atachaguliwa kuongoza taasisi hiyo, ataweka msisitizo katika kuimarisha sekta ya afya barani Afrika kwa kushirikiana na nchi wanachama wa SADC Kujenga Afrika yenye afya kwa pamoja.