Na.Samwel Mtuwa – Kahama
Mgodi wa uchimbaji na uzalishaji wa madini ya dhahabu wa Bulyanhulu uliopo kahama mkoani Shinyanga umetakiwa kutenga fedha za afya na masuala yanayohusu UKIMWI kupitia Mpango wa Ushirikishaji Jamii inayozunguka mgodi (CSR).
Hayo yameelezwa leo Machi 16, 2025 na Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI ilipotembelea mgodi huo kwa lengo la kukagua na kupata taarifa za utekelezaji wa afua za afya na UKIMWI mgodini.
Dkt.Kiruswa ameieleza menejimenti ya mgodi huo kuwa Serikali kupitia wizara ya madini imetunga kanuni zinazohusu kutenga fedha kwa ajili ya miradi ya afya kwa jamii inayozunguka mgodi hususan katika masuala ya afya kwa magonjwa yanayoambukiza na yasioambukiza.
Akifafanua kuhusu kuwepo kwa miradi ya afya na masuala ya UKIMWI mgodini, Dkt. Kiruswa amesema kuwa, kutengwa fedha kwa ajili ya CSR katika masuala ya afya hususan katika magonjwa sugu yanayoambukiza na yasiyo ambukiza kutasaidia katika kuboresha huduma za afya, kuzuia magonjwa kuenea kwa kasi, kutoa elimu kwa jamii kuhusu afya pamoja na kutoa msaada kwa vituo vya afya vinavyozunguka mgodi.
Awali, akiongea katika kikao cha kuikaribisha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha ameupongeza mgodi wa Bulyanhulu kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya jamii ikiwemo miradi ya maji, barabara , elimu na kilimo na kuwataka waendelee na juhudi hizohizo kwa manufaa ya taifa.
Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI, Hassan Mtenga ameuelekeza mgodi kufanya maboresho yote yaliyotolewa na Wajumbe wa Kamati kuhusu ufuatiliaji, uboreshaji wa masuala yote yanayohusiana na afua za afya kwa magonjwa yanayoambukiza na yale yasioambukiza ili kuuweka mgodi katika huduma bora za afya kwa jamii.
Akielezea kuhusu mwenendo wa maambukizi ya virus vya Ukimwi sehemu za migodi , Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la kupambana na maambukizi ya Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Dkt. Catherine Joachim amesema kuwa, kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2024 takwimu zinaonesha watu milioni 1.7 wanaishi na virus vya ukimwi wakati mwaka wa 2022/2023 utafiti ulionesha watu elfu 60 waliambukizwa virusi vya UKIMWI, ambapo sehemu za mgodini zimetambulika kama sehemu hatarishi.
Naye , Meneja Mkuu wa mgodi huo , Victor Lule ameishukuru kamati ya bunge kwa mawazo chanya waliyotoa kwa mgodi na kuahidi kuwa ushauri wote uliotolewa utafanyiwa kazi kwa asilimia 100 kupitia idara husika za mgodi , kwa kuzingatia kanuni , taratibu na Mpango wa CSR unavyoelekeza.