Na Neema Mtuka Sumbawanga,
Rukwa :Mbunge wa jimbo la Sumbawanga mjini, Aesh Hilaly amesema ataibana Serikali ili ijenge Meli katika ziwa Tanganyika hali itakayosaidia kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mizigo katika ziwa hilo.
Mbunge Aesh alisema pia uwepo wa meli hiyo, utasaidia kupunguza vipo vya watu wengi wanatumia usafiri wa majini katika ziwa hilo linalounganisha mikoa ya Kigoma Katavi na Rukwa kwa upande wa Tanzania.
Alisema hayo jana jioni katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Kirando wilayani Nkasi ambako aliambatana na mwenyekiti wa CCM mkoa Sirafu Maufi ambao wote walitumia fursa hiyo kueleza utekelezaji wa ilani ya CCM.
“Ndugu zetu wengi wanafariki dunia katika ziwa Tanganyika kutokana na kukosa usafiri wa uhakika wa meli hivyo nitapambana kuhakikisha tunapata meli ambayo itakuwa msaada kwetu na chachu ya maendeleo ya mikoa hiyo”.
Katika nyingine alitoa fedha kiasi cha Shilingi milioni tano kuchangia ujenzi wa Zahanati ya Mpata ili wananchi waweze kupata huduma za afya, tofauti na sasa ambapo wanalazimika kutembea umbali mrefu kutatufa huduma hizo.
Alitoa msaada huo kufuatia ombi la Diwani aliyejiondoa Chadema na kujiunga na Ccm, Sebastian Kakuli kumweleza mbunge huyo kuhusu kero za upatikanaji wa huduma za afya katika eneo hilo.
Aidha, akiwahutubia wananchi hao, Aeshi alizungumza kero ya ukosefu wa Mochwari katika kituo cha afya Kirando ambapo alimtaka mwenyekiti kutoa maagizo ya ujenzi wa jengo la kuhifadhia maiti kwa kuwa ni kero.
Alisema atapigania uuzaji mazao ya mahindi, akitaka Serikali iwape uhuru wakulima kuchagua wanalotaka hivyo kutofunga mipaka kama inavyofanyika ivi sasa.
“Mwaka huu tunategemea kuvuna mazao mengi ya mahindi ivyo hakuna sababu ya kufunga mipaka, tuache wakulima watafute soko nje nchi na kujipatia kipato kikubwa” alisema