Na Mwandishi wetu, Mirerani
KAMATI ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, imeridhishwa na mradi wa ujenzi wa soko la madini ya Tanzanite lililopo mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Timotheo Mnzava akizingumza baada ya kutembelea na kukagua jengo hilo amesema hii ni mara ya pili wao kufika hapo kwani walifika kwa mara ya kwanza mwaka 2023.
Mnzava amesema kamati hiyo imeridhishwa na ulipaji fidia kwa baadhi ya watu waliokuwa wakiishi maeneo hayo na kupisha ujenzi wa jengo hilo kupatiwa haki zao.
“Tunatarajia mradi huu utakamilika kwa wakati na kuanza kufanyiwa kazi kwani sababu na umuhimu wa jengo hili inajuliana hivyo baada ya sakafu mbili kukamilika hizo nyingine tatu nazo zikamilishwe,” amesema Mnzava.
Mbunge wa vijana Taifa Asia Halamga amesema jengo hilo likikamilika itakuwa ni miongoni mwa jitihada za dhati za serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwajali watu wa mkoa wa Manyara.
“Jengo hili litaongeza hali ya uchumi mzuri katika eneo la Mirerani, Simanjiro na Manyara kwa ujumla hivyo jitihada za dhati zifanyike ili wapatiwe fedha za kukamilisha jengo hili kwani huwezi kunawa uso nusu,” amesema Halamga.
Mkurugenzi wa ujenzi wa shirika la nyumba la Taifa (NHC) Dkt Godwin Maro amesema mkataba wa ujenzi wanatarajia kukamilisha mwez huu wa Machi 2025.
Dk Maro amesema kazi za ujenzi zilizopo kwenye mkataba wa sasa zimefikia asilimia 95.
Amesema kazi zinazoendelea kwa sasa ni umaliziaji wa uwekaji wa milango, marumaru, mifumo ya maji safi na taka,, umeme na upandaji maua.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geoffrey Pinda amesema wamepokea maelekezo yote ya kamati na wanatarajia kuyatekeleza kwa wakati.
Pinda amesema wanaipongeza kamati hiyo kwa kufanya ziara kwenye jengo hilo ambalo ni mali ya halmashauri ya wilaya ya Simanjiro na linajengwa na NHC.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Fakii Raphael Lulandala amesema maendeleo makubwa yatapatikana kupitia jengo hilo lililopo eneo la Tanzanite city pindi likikamilika.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Gracian Makota amewaalika wadau wote wenye kutaka kuwekeza jirani na jengo hilo kuwasiliana na ofisi yake.


