Mkutano wa Mawaziri wa Majadiliano ya Ushirikiano kati ya Jumuiya ya Maendekeo Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Ulaya (EU) umefanyika Machi, 15, 2025 jijjini Harare, Zimbabwe, ambapo Jumuiya hizi mbili zimejadili na kukubaliana kuendelea kushirikiana katika masuala ya mbalimbali ikiwemo kuimarisha amani na usalama, kuhamasisha maendeleo endelevu, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, mazingira na kukuza biashara na uwekezaji.
Mkutano huo umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara za Kimataifa wa Zimbabwe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa SADC, Mhe. Prof. Amon Murwira kama Mwenyekiti Mwenza akishirikiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland, Mhe. Radoslaw Sikorski, akimwakilisha Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia masuala ya Mambo ya Nje katika Kamisheni ya EU.
Majadiliano hayo ambayo yalianza rasmi mwaka 1994, hutumika kama jukwaa la kuimarisha ushirikiano baina ya SADC na EU hususan katika kukuza ushirikiano katika masuala ya amani na usalama, na sera za biashara zinazolenga katika mageuzi ya kiuchumi ili kuwa na uchumi endelevu katika Kanda ya SADC.
Aidha, wakati wa majadiliano hayo wajumbe walipata fursa ya kupitia utekelezaji wa makubaliano mbalimbali yaliyofikiwa baina ya Jumuiya hizi mbili hususan kupitia Mpango wa miaka mitano wa ushirikiano wa EU na Nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara (MIP SSA) wa kuanzia mwaka 2021-2027.
Kadhalika wajumbe wa mkutano huo walishuhudia kusainiwa kwa mikataba nane ya ushirikiano yenye thamani ya Euro Milioni 163.9 kwa ajili ya kufadhili program mbalimbali za kanda ya kusini mwa Afrika ikiwemo masuala ya amani na usalama, biashara na usafirishaji, usimamizi wa maliasili, mifumo ya kilimo na chakula, mageuzi katika masuala ya kidijitali na kuzijengea uwezo taasisi mbalimbali.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umeongozwa na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Mhe. Omar Said Shaaban ambapo pia umemjumuisha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Hassan Serera, Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na Mwakilishi katika Umoja wa Ulaya, Mhe. Jestus Nyamanga, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga, Mratibu wa Kitaifa wa masuala ya SADC ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri na Maafisa Waandamizi kutoka Serikalini.
Katika mkutano huo, SADC imewakilishwa na Nchi sita zinazounda Utatu wa Asasi Mbili za SADC (SADC Double-Troika) ambazo ni Zimbabwe (Mwenyekiti wa SADC), Angola (Mwenyekiti aliyemaliza) na Madagascar (Mwenyekiti ajaye). Nchi nyingine ni zile tatu zinazounda Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama yaani Tanzania (Mwenyekiti), Malawi (Mwenyekiti ajaye) na Zambia (Mwenyekiti aliyemaliza).