Na John Walter -Babati
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) imefanya ziara mkoani Manyara kwa ajili ya kukagua miradi ya maendeleo inayosimamiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Katika ziara hiyo, kamati ilitembelea na kukagua ujenzi wa jengo la ofisi ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani humo, ambalo linaendelea kujengwa katika Kata ya Maisaka, eneo la Katani.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, ameieleza kamati kuwa pato la mkoa huo, ambao unajikita katika sekta za kilimo, ufugaji na utalii, limeendelea kuimarika.
Pia amebainisha kuwa hali ya ulinzi na usalama mkoani humo imeendelea kuimarika, huku changamoto kubwa ikiwa ni msongamano wa mahabusu kwenye magereza.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Paul Mbogo, amesema kamati imepokea changamoto zilizowasilishwa na kwamba zitafanyiwa kazi katika bajeti ijayo ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kuleta manufaa kwa wananchi.
Jengo la Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Manyara litakuwa na sakafu mbili na litajumuisha ofisi saba, zikiwemo ofisi za Kamanda wa Mkoa, Kamanda wa Wilaya, Mhasibu na Masijala.
Pia, litakuwa na magari matatu yenye mitambo ya kisasa ya kuzima moto ili kuhakikisha huduma za uokoaji zinaboreshwa katika mkoa huo.
Kwa mujibu wa taarifa, gharama za ujenzi wa jengo hilo hadi kukamilika kwake ni shilingi milioni 600.6, na hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 48.2.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo, amepongeza hatua ya ujenzi ilipofikia na kusisitiza kuwa kukamilika kwake kutarahisisha shughuli za uokoaji wakati wa majanga, hivyo kuokoa maisha na mali za wananchi.
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, John Masunga (CDF), amesema jengo hilo litakuwa na mifumo ya kisasa ya TEHAMA, na linatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 30 Juni 2025.
Aidha, Masunga alibainisha kuwa kituo hicho ni sehemu ya miradi saba ya ujenzi wa vituo vikubwa vya zimamoto vinavyojengwa katika mikoa ambayo awali haikuwa na vituo vikubwa vya huduma hiyo.
Ameeleza kuwa lengo ni kusogeza huduma kwa wananchi na kuhakikisha kila mkoa unakuwa na kituo cha kisasa cha zimamoto na uokoaji.
Jeshi hilo kwa sasa lipo kwenye wilaya 25 na linaendelea na mpango wa kupanua huduma ili kuzifikia wilaya zote nchini.
Mpango huo unakwenda sambamba na ununuzi wa vifaa vya kisasa vya zimamoto na uokoaji ili kuboresha utendaji kazi wa jeshi hilo.
Kamati hiyo imeishukuru Serikali kwa kutenga fedha za umaliziaji wa vituo hivyo na imewataka makamanda wa mikoa kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati.