Mbunge wa Jimbo la Kilombero, Mhe. Abubakary Asenga, amesema kuwa juhudi za kutoa elimu kuhusu matumizi salama ya mitandao zimeleta mafanikio makubwa katika kupunguza vitendo vya utapeli katika Wilaya ya Ifakara.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mhe. Asenga alisema kuwa baada ya viongozi wa vijiji na vyama vya siasa kupatiwa mafunzo ya matumizi salama ya mitandao, wananchi wa Ifakara wameweza kujilinda dhidi ya matapeli waliokuwa wakitumia ujumbe wa maandishi (SMS) wa udanganyifu ili kuwaibia fedha kupitia simu za mkononi.
Mbunge huyo alieleza kuwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilitoa semina maalum kwa viongozi hao, hatua ambayo imesaidia kupunguza vitendo vya uhalifu wa kimtandao.
“Kwa sasa, hali ya usalama wa mitandao Ifakara imeimarika. Zamani utapeli kupitia simu za mkononi ulikuwa umeshamiri, ambapo wananchi walikuwa wakipokea ujumbe wa kuwataka watume fedha kwa namba fulani. Lakini sasa, baada ya kupatiwa elimu, wamekuwa makini na hawaingii katika mtego wa matapeli,” alisema Mhe. Asenga.
Mbunge huyo aliwahimiza vijana kuendelea kujikita katika shughuli za kiuchumi kama kilimo na usafirishaji wa abiria kwa bodaboda, huku akiwataka kuwa waangalifu wanapotumia mitandao ya kijamii ili kuepuka kuathiriwa na matapeli.
Pia alitoa wito kwa wananchi kuepuka kufungua viunganishi vya tovuti (links) kutoka kwa watu wasioaminika, kwani matapeli hutumia mbinu hizo kupata taarifa binafsi za watu na kufanya vitendo vya uhalifu wa kimtandao.