Mkutano wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umemalizika Machi 14, 2025 jijini Harare, Zimbabwe huku viongozi hao wakiazimia kutekeleza kwa vitendo agenda za kipaumbele za kujikwamua kiuchumi katika kanda.
Mkutano huo ambao ulitanguliwa na vikao mbalimbali ikiwemo Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu, pamoja na mambo mengine umejadili na kupitisha agenda mbalimbali ikiwemo tathmini ya utekelezaji wa Maamuzi ya Baraza na yale ya Wakuu wa Nchi na Serikali pia mkutano huo umetathmini utekelezaji wa Mpango wa Bajeti ya Jumuiya ya Mwaka wa Fedha 2024/2025 na kuweka mikakati ya utekelezaji wa mipango ya mwaka wa fedha 20225/2026 hususan katika maeneo ya kipaumbele yaliyoainishwa kwenye Mpango Mkakati wa Maendeleo wa Kanda (RISDP) wa mwaka 2020-2030 yanayosisitiza katika kuharakisha maendeleo ya viwanda na miundombinu ya kuiunganisha kanda.
Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo uliongozwa na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Mhe. Omar Said Shaaban ambapo agenda za Tanzania za kipaumbele katika Mkutano huo ikiwa ni pamoja na kuhimiza kufanyika kwa tafsiri ya nyaraka muhimu za SADC katika Lugha ya Kiswahili baada ya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya SADC zikipitishwa.
Akihitimisha Mkutano huo, Mwenyekiti wa Baraza ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara za Kimataifa wa Zimbabwe, Mhe. Prof. Dkt. Amon Murwira amesema makubaliano na maamuzi yaliyofikiwa wakati wa mkutano huo yanadhihirisha dhamira ya pamoja iliyopo miongoni mwa Nchi Wanachama wa SADC ya kushirikiana katika kuiletea maendeleo endelevu kanda ya SADC.
Amesema ili kanda ya SADC ifikie mafanikio yaliyokusudiwa ni muhimu kutoa kipaumbele katika utekelezaji wa maamuzi kwa kuhakikisha maneno yanatafsiriwa kwa vitendo ili kuwawezesha raia katika nchi wanachama wa SADC kufaidika na mtangamano huu wa kikanda.
“Wakati wa Mkutano wetu tumejadili masuala mengi ikwemoa amani na usalama na mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa mipango yetu ya maendeleo hususan iliyopo katika Mpango Mkakati wa Maendeleo wa Kanda (RISDP) wa mwaka 2020-2030. Jambo muhimu ni kutafsiri changamoto hizo kama fursa ya kujifunza na kuandaa mikakati mipya ya kukabiliana nazo” alisema Prof. Murwira.
Mbali na Waziri Shaaban, ujumbe wa Tanzania ulimjumuisha pia Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Hassan Serera, Mratibu wa Kitaifa wa masuala ya SADC ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri na Maafisa Waandamizi kutoka Serikalini.
Baraza la Mawaziri ni chombo muhimu katika SADC ambacho kinahusika na kusimamia uendeshaji wa SADC ili kuhakikisha sera na maamuzi mbalimbali yanayofikiwa kwenye vikao yanafanyiwa kazi ipasavyo. Baraza hili linaundwa na Mawaziri kutoka Nchi Wanachama 16 za SADC, hususan kutoka katika Wizara zinazoshughulikia masuala ya Mambo ya Nje, Mipango na Fedha au Biashara, na hukutana mara mbili kwa mwaka.