Mkurugenzi wa Rasilimali watu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Brigedia Jenerali Simon Pigapiga amefunga rasmi mafunzo ya Mchezo wa Soka la Ufukweni yaliyoendeshwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa Wanajeshi wa JWTZ Katika Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa Mbweni leo tarehe 14 Machi 25.
Akimwakilisha Mkuu wa Utumishi Jeshini Meja Jenerali Marco Gaguti, Brigedia Jenerali Pigapiga amewataka wahitimu wa mchezo huo kutumia mafunzo hayo kwa kuwafunza Maafisa na Askari wengine wa JWTZ ili mchezo huo uwe na tija katika mashindano mbalimbali Jeshini.
Aidha, Brigedia Jenerali Pigapiga ameshukuru Uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini kwa usimamizi wa mafunzo hayo.
Akizungumza kwa niaba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu(TFF), Rais wa Shirikisho Bw. Wallace Karia, amesema, Tff inaendelea kushirikiana na JWTZ katika kukuza na kuinua mchezo wa soka nchini, na kuwaomba wahitimu wa mafunzo haya kutumia elimu na maarifa ya mchezo wa Soka la Ufukweni kuwafunza maafisa na Askari katika maeneo wanayotoka. Pia, Bw. Karia amemshukuru Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob Mkunda kwa kupokea wazo la kuanzishwa mchezo wa Soka la Ufukweni kwani unaonekana kuwa na manufaa kwa jeshi na taifa kwa ujumla.
Mafunzo ya Mchezo wa Soka la Ufukweni kwa Maafisa na Askari wa JWTZ umewezesha jeshi kuwa na wachezaji na wakufunzi wa mchezo huo ambao watatumika kuunda timu katika jeshi na kuunda timu ya taifa chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), huku miundombinu ya mchezo huo iliyopo katika Kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa Mbweni, ikionekana kuendelea kuimarika, na ujenzi unaendelea.
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa kushirikiana na Shirikisho la mpira wa miguu nchini limedhamiria kuukuza na kuendeleza mchezo wa Soka la Ufukweni kwa kuandaa wachezaji wanajeshi watakaoweza kuitumikia timu ya taifa ya Soka la Ufukweni katika michuano mbalimbali ndani na nje ya bara la Afrika.