Harare, Zimbabwe – 13 Machi 2025
Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wamekutana katika Mkutano Maalum kujadili hali ya usalama inayozidi kuzorota katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Mkutano huo, uliofanyika tarehe 13 Machi 2025, uliongozwa na Mwenyekiti wa SADC, Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mheshimiwa Dk. Emmerson Dambudzo Mnangagwa.
Mkutano huo ambao umefanyika kwa njia ya mtandao ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa nchi wanachama wa SADC au wawakilishi wao, akiwemo Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mheshimiwa Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan, na viongozi wengine kutoka Botswana, Madagascar, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Zambia, Lesotho, Eswatini, Malawi, Mauritius, Angola, na Ushelisheli.
Katika mkutano huo, viongozi walipokea taarifa za hali ya usalama Mashariki mwa DRC, ikiwa ni pamoja na Ripoti ya Ujumbe wa SADC nchini humo (SAMIDRC), kufuatia Mkutano Maalum wa Troika ya SADC uliofanyika tarehe 6 Machi 2025.
Viongozi wa SADC walitoa salamu za rambirambi kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Afrika Kusini, Malawi, na Tanzania, pamoja na familia za wanajeshi waliopoteza maisha wakihudumu chini ya SAMIDRC. Aidha, waliwatakia ahueni ya haraka wale waliojeruhiwa.
Pamoja na hayo, mkutano ulieleza wasiwasi mkubwa juu ya hali mbaya ya usalama Mashariki mwa DRC, ikiwemo kutekwa kwa miji ya Goma na Bukavu na kuzuiliwa kwa njia kuu za usafirishaji misaada ya kibinadamu. Viongozi walipongeza wanajeshi waliopo DRC kwa ujasiri wao katika kulinda amani na kusisitiza umuhimu wa kulinda raia na kuhakikisha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu bila vikwazo.
Aidha, mkutano ulitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa, ikiwemo Umoja wa Mataifa (UN) na Umoja wa Afrika (AU), kusaidia juhudi za misaada ya kibinadamu kwa wananchi wa DRC.
Katika hatua nyingine, viongozi wa SADC walitangaza kusitishwa rasmi kwa mamlaka ya Ujumbe wa SAMIDRC na kuagiza kuanza kwa uondoaji wa vikosi hivyo kwa awamu.
Mkutano huo pia ulisisitiza umuhimu wa kutafuta suluhisho la kisiasa na kidiplomasia kwa mgogoro wa DRC, likihusisha pande zote, zikiwemo serikali, makundi yasiyo ya kiserikali, wanajeshi, na raia, kwa ajili ya kurejesha amani na utulivu katika nchi hiyo.
Viongozi wa SADC walikubaliana pia kuunganisha mchakato wa Luanda na Nairobi ili kuongeza ufanisi wa juhudi za upatanishi, huku wakikubali Azimio 2773 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC), linaloelekeza njia ya suluhisho la kudumu kwa mgogoro huo.
Katika hotuba yake, Rais wa DRC, Mheshimiwa Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo, aliishukuru SADC kwa kuendelea kusaidia juhudi za kurejesha amani nchini mwake.
Mkutano huo ulimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa mchango wake katika kusimamia masuala ya amani na usalama ndani ya kanda ya SADC. Pia, viongozi walimshukuru Mwenyekiti wa SADC, Rais Dk. Emmerson Mnangagwa, kwa kuitisha mkutano huo na kuendelea kushirikiana katika kuhakikisha amani, usalama, na maendeleo ya kikanda yanadumishwa.
Mkutano huo ulifanyika kwa njia ya mtandao na kuhitimishwa kwa wito wa mshikamano wa kikanda katika kukabiliana na changamoto za usalama zinazoikabili DRC na nchi nyingine za SADC.