FARIDA MANGUBE, MOROGORO
Baraza la Vyama vya Siasa nchini limekemea vikali baadhi ya vyama vya siasa kwa kutumia vibaya majukwaa na mikutano ya kisiasa kuhamasisha uvunjifu wa Katiba na sheria za nchi.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari katika kikao cha kawaida cha Baraza hilo, Mwenyekiti wa Baraza Juma Ally Khatibu, amesema kuwa Baraza halitawavumilia wanasiasa wanaotumia majukwaa ya kisiasa kuhamasisha vurugu na uvunjifu wa amani.
Aidha, Mwenyekiti huyo amesisitiza kuwa, wakati taifa likielekea katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge, na Madiwani mwezi Oktoba mwaka huu, Baraza halitafumbia macho wanasiasa watakaohamasisha wananchi kukiuka misingi ya Katiba na maadili ya Kitanzania.
Hata hivyo, Baraza hilo limevitaka vyama vyote vya siasa nchini kuheshimu Katiba, sheria za nchi, na maadili ya uchaguzi, sambamba na kudumisha amani na utulivu uliopo.
Kwa upande wao, baadhi ya wajumbe wa Baraza hilo, wakizungumza baada ya kikao hicho, wameeleza kushangazwa na hatua ya chama cha ACT Wazalendo kuchapisha na kusambaza kipeperushi kinachobeza shughuli za Baraza hilo na baadaye kutoshiriki kikao kilichoandaliwa.
Katibu Mkuu wa chama cha National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo, amesema kuwa ACT Wazalendo ni miongoni mwa vyama vilivyopata msaada mkubwa kutoka Baraza hilo tangu kilipoanzishwa, hivyo hakukuwa na sababu ya kubeza kazi zake.
Naye Katibu Mkuu wa chama cha Democratic Party (DP), ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa na Bunge, Abdul Mluya, amesema kuwa Baraza limekuwa kiunganishi muhimu kati ya vyama vya siasa na serikali katika masuala mbalimbali yahusuyo vyama hivyo.
Aidha, ameeleza kuwa kitendo cha ACT Wazalendo kuchapisha ujumbe unaolenga kudhalilisha chombo kilichoundwa kisheria si jambo la kufumbiwa macho. Ameongeza kuwa, kutokana na chama hicho kuwa kichanga ukilinganisha na vyama vingine, hakipaswi kulaumiwa sana, bali kinapaswa kuelekezwa ili kifahamu umuhimu wa kuheshimu taasisi rasmi za kisiasa nchini