Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, ameongoza hatua muhimu katika maboresho ya huduma kwa wateja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kuzindua namba ya bure ya huduma kwa wateja – 180. Uzinduzi huu unalenga kurahisisha mawasiliano kati ya TANESCO na wateja wake, huku ukihakikisha changamoto zinatatuliwa kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.
Hatua hii ni utekelezaji wa agizo la Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, aliyesisitiza umuhimu wa kuwa na namba ya bure kwa wateja ili kuboresha utoaji wa huduma. Kupitia namba hii, wateja wa TANESCO wataweza kupata msaada wa haraka kuhusu matatizo ya umeme, bili, na huduma nyinginezo bila gharama yoyote.
Akizungumza mara baada ya kuzindua huduma hiyo, Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga aliwataka Mameneja wa Mikoa na Wilaya wa TANESCO kuhakikisha huduma kwa wateja inaboreshwa kupitia usimamizi madhubuti wa mfumo huo mpya. Pia aliwahimiza wananchi kuitumia namba hiyo kwa malengo sahihi, akisisitiza kuwa serikali ya Awamu ya Sita inajidhatiti kuhakikisha huduma za umeme zinapatikana kwa uhakika na ubora.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Balozi Zuhura Bundala, alieleza kuwa maboresho ya huduma kwa wateja ni moja ya vipaumbele vya shirika hilo, kwani maendeleo ya kiuchumi yanategemea upatikanaji wa umeme wa uhakika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mha. Gissima-Nyamo Hanga, alisema kuwa katika dunia ya sasa ya ushindani wa kibiashara, ni muhimu kuhakikisha wateja wanapata huduma bora na changamoto zao zinatatuliwa kwa haraka.
Uzinduzi wa namba hii ya bure ni moja ya juhudi za TANESCO kuboresha huduma kwa wateja wake na kuimarisha mfumo wa mawasiliano na wananchi.