Mwamvua Mwinyi, Pwani
Machi 11, 2025
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, asisitiza Viongozi na Watendaji wa Halmashauri Kuzingatia Misingi ya Haki, Kanuni, na Sheria za Utawala Bora ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi
Rai hiyo aliitoa wakati akifungua mafunzo ya siku moja kuhusu Elimu ya Uraia, Utawala Bora, na Haki za Binadamu kwa viongozi wa Halmashauri za Mkoa wa Pwani, Mafunzo hayo ambayo yameratibiwa na Wizara ya Katiba na Sheria na kufanyika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Kibaha.
Kunenge alieleza kuwa ili kuboresha maisha ya wananchi, viongozi lazima waongozwe na misingi ya haki, sheria, na kanuni za utawala bora.
Aliongeza ,ni muhimu kwa viongozi kuwa na dhamira ya dhati ya kubadilisha hali ya maisha ya wananchi.
“Serikali imejizatiti kutoa mafunzo haya ili tuwadumishe wananchi kwa kufuata misingi ya haki na kanuni za utawala bora, Lazima tusikilize wananchi kabla ya kufanya maamuzi, Wajibu wenu ni kujifunza na kuleta matokeo chanya kwani Tutajipima kwa kuona wananchi wangapi wanaridhika na utendaji wetu,” alieleza Kunenge.
Kunenge alieleza pia kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha wananchi wanapata uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya utawala bora, haki za binadamu, ukatili wa kijinsia, na umuhimu wa uwajibikaji wa viongozi kwa jamii.
“Viongozi lazima waelewe kuwa kazi yao siyo tu kutoa huduma, bali pia kusikiliza na kujua changamoto za wananchi wao kabla ya kufanya maamuzi, Ni muhimu kufanya kazi kwa ufanisi kwa kutambua vipaumbele na kuwa na dhamira ya kuboresha maisha ya watu,” alieleza Kunenge.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Katiba na Ufuatiliaji Haki, Lawrence Kabigi, alisisitiza umuhimu wa umakini katika utekelezaji wa majukumu ya kila mtumishi wa umma.
“Matarajio ya Wizara ni kwamba, baada ya mafunzo haya, viongozi mtaweza kuzingatia haki za binadamu, kutekeleza utawala bora, na kutambua maadili ya utendaji kazi, Hili litasaidia kuhakikisha kuwa viongozi wanakuwa na ufanisi na wanatoa huduma bora kwa wananchi,” alisema Kabigi.
Mada zilizozungumziwa katika Mafunzo hayo zilijikita katika utawala wa sheria, uwajibikaji, ushirikishwaji wa wananchi katika maamuzi, na umuhimu wa kuheshimu haki za binadamu katika utendaji kazi za Serikali.