Na. Nancy Kivuyo, VIWANDANI
Walimu watakiwa kudhibiti matumizi mabaya ya ‘internet’ kwa wanafunzi shuleni ili kukabiliana na mabadiliko makubwa ya utandawazi na matumizi ya teknolojia.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri wakati wa Hafla ya Ugawaji wa Kompyuta na Printa kwa Shule za Sekondari za Serikali jijini Dodoma, iliyofanyika katika Shule ya Sekondari Viwandani.
“Rai yangu ni kwamba tujitahidi kuweka ‘internet’ ili kusudi matumizi chanya kabisa ya maabara hiyo iweze kufanyika. Tukishaweka hiyo ‘internet’ tusisahau kuweka udhibiti ili vijana wetu wawe salama na matumizi yasiyo rafiki ya mitandao. Bahati mbaya wapo vijana wanaotumia mitandao kupenyeza agenda husuani mitaala ambayo haifai kwenye elimu yetu, kwahiyo ili kuzuia hayo ni muhimu kuweka vidhibiti na kuwa makini” alisema Alhaj Shekimweri.
Nae, Mwalimu wa Shule ya Sekondari Viwandani, Mwl. Dickson Massatu, alieleza kuwa amefurahi Shule ya Sekondari Viwandani kupatiwa vifaa hivyo kwasababu vitawasaidia katika kuendeleza ufanisi shuleni hapo.
“Kompyuta zinatusaidia sana sisi walimu kupata nafasi ya kuperuzi taarifa nyingi hasa za kitaaluma na kuongeza wigo wa ubunifu katika kufundisha. Pia wanafaunzi watafaidika sana kwani watapata masomo mengi ikiwa pamoja na mitihani ya kujipima hivyo ninaamini ufaulu utaongezeka” alisema Mwl. Massatu.
Katika hatua nyingine mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Viwandani, Careen Busungu, alishukuru Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini kuwaboreshea maabara ya kompyuta na wanaahidi kuitumia vizuri kama ilivyoelekezwa.
“Tunamshukuru sana mbunge, ameona tunastahili kupata kompyuta na printa shuleni kwetu ili kurahisishia namna ya kusoma, nawashauri wanafunzi wenzangu tuzingatie matumizi mazuri ya kompyuta tulizopewa ili ziturahisishie masomo” alisema Busungu.