*Uwekaji saini wa ujenzi wa Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Kilimanjaro
(KMICC) kati ya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ni kielelezo cha utekelezaji wa maono ya Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan.
Hayo yammeelezwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb) wakati wa hafla ya uwekaji saini wa Ukumbi huo utakao kuwa mkubwa zaidi nchini iliyofanyika jijini Arusha Machi 08,2025.
“Mhe. Rais Samia ameona kwa uono mpana kabisa kuna fursa nyingi katika utalii wa vikao, incentives, mikutano na maonesho (meetings, incentives, conferences and exhibition-MICE) ambazo hazijatumiwa vizuri kutokana na miundombinu duni, hivyo, ujenzi wa ukumbi huu ambapo ammeelekeza pia ijengwe na hoteli isiyopungua ya vyumba 500 pembezoni mwa ukumbi ni mwendelezo wa Serikali yake wa kutatua changamoto katika sekta ya utalii”, Balozi Kombo alisema.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali waandamizi wa Serikali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu kazi vijana, ajira na wenye ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb) ametoa wito kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii PSSF na AICC kuhakikisha wanasimamia vyema mradi wa ujenzi wa ukumbi huo utakao kuwa na uwezo wa kubeba watu 5,000 kwa mara moja.
Amesema mchakato wa ujenzi wa kituo hicho ni matokeo ya miongozo mbalimbali inayoongozwa na dira ya taifa ya maendeleo ya mwaka 2025.
“Utekelezaji huu ni maelekezo ya ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi ya mwaka 2020 hadi 2025 inayotuelekeza kujenga ukumbi mkubwa wa mikutano utakaoweza kuileta Dunia Tanzania”, Amesema.
Aidha, amesema anafarijika kuona taasisi ya PSSF ilivyoingia makubaliano mazuri na kituo cha Mikutano cha AICC katika utekelezaji wa mradi huu ambao unatakiwa kukamilika katika kipindi cha miaka miwili.
“Nitahakikisha mradi huu unakamilika kama ambavyo tumekubaliana kwenye mkataba ili uweze kuleta tija kwa Watanzania”
Aliongeza kuwa Mradi huo ni wa kujivunia kwani unakwenda kuweka alama kubwa Tanzania na unajengwa na watanzania wenyewe na utasaidia kuchochea fursa za kiuchumi katika mji wa Arusha na Tanzania kwa ujumla.