Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akibonyeza kitufe kuashiria ufunguzi wa mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe mara baada ya kuhutubia wananchi wa wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro tarehe 09 Machi, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kukamilika kwa Mradi wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe ni ukombozi kwa wananchi katika Wilaya za Same, Mwanga na Korogwe.
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo wakati akizungumza na wakazi wa Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro mara baada ya kuzindua rasmi Mradi wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe.
Taarifa iliyotolewa na Sharifa B. Nyanga Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu imesema Rais Dkt. Samia amefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Mkoa wa Kilimanjaro ambapo alifika kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu kuweka jiwe la msingi la mradi huo.
Rais Dkt. Samia amesema mradi huo umeongeza uwezo wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Same-Mwanga kufikisha maji safi na salama kwa wananchi kutoka watu 50,615 hadi 300,000 kwenye vijiji 38 katika Wilaya za Same, Mwanga na Korogwe.
Akizungumzia jitihada kubwa zilizofanyika kuukwamua mradi huo na kuhakikisha wananchi wanapata maji, Rais Dkt. Samia amesema haamini katika kushindwa, na amewarai watumishi wa umma kuwa na moyo wa kupambana katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Aidha, Rais Dkt. Samia ameitaka Wizara ya Maji kuhakikisha awamu ya pili ya mradi huo inatekelezwa kwa ukamilifu ili kuimarisha upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Korogwe.
Vilevile, Rais Dkt. Samia amesisitiza uwajibikaji kwa watumishi wa sekta ya maji, hususan katika kuhakikisha huduma ya naji safi na salama inakuwa endelevu katika maeneo ambako miundombinu ya maji imefika.
Aidha, Rais Dkt. Samia amewataka watumishi wa sekta ya maji kuwahudumia wananchi kwa weledi na kwa wakati na kulinda vyanzo vya maji ili kuwezesha Serikali kutimiza ahadi yake kwa wananchi.
Sehemu ya wananchi wa Mwanga pamoja na wageni mbalimbali wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan uliofanyika Mwanga mkoani Kilimanjaro tarehe 09 Machi, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwahutubia wananchi wa Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro mara baada ya kuzindua mradi wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe, tarehe 09 Machi, 2025.