Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali leo tarehe 8 Machi, 2025 imeshiriki Maadhimisho ya Siku ya Wanawake duniani mkoani Dodoma, kwa kushiriki katika maandamano yaliyoanzia katika Viwanja vya Nyerere Square hadi Viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri mewapongeza Wanawake kwa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake duniani, huku akisisitiza kuwathamini na kuwajali wanawake kwani ni nguzo muhimu katika kukuza maadili na Uchumi wa familia na Taifa kwa ujumla.
“Niwapongeze sana akina mama kwa kuadhimisha siku yenu adhimu ambayo imekuwa chachu ya kuwainua Wanawake katika kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo na kijamii.”
Kwa upande wake, Mpokezi Mwandamizi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bi. Rehema Msemwa amesema kuwa ushiriki wa Wanawake katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake duniani ni nafasi kwa Wanawake kuweza kukutana na kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu wanawake katika Nyanja za kiuchumi na Kijamii.
“Naushukuru sana uongozi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutuwezesha Wanawake kushiriki katika maadhimisho haya kwetu ni nafasi muhimu ya kukutana na Wanawake wenzetu na kuweza kukumbushana mambo mbalimbali yatakayotuwezesha kujikwamua kiuchumi na kijamii.” Amesema Bi. Rehema
Nae, Mtunza Kumbukumbu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bi. Grace ameuopongeza Uongozi na Menejimenti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuwawezesha wanawake kushiriki katika maadhimisho hayo, ambapo amesema uongozi umeonyesha namna unavyowathamini wanawake katika Ofisi hiyo.
“Leo tumeshiriki katika maadhimisho haya kwa kufanya maandamano kuanzia Nyerere Square hadi hapa Chinangali, tunashukuru uongozi wetu kwa kututhamini na kutuwezesha kushiriki katika siku hii.” Amesema Bi Grace
Siku ya Wanawake duniani huadhimishwa tarehe 8 Machi kila Mwaka, ambapo kwa mwaka huu Maadhimisho ya Siku ya Wanawake duniani kitaifa yanafanyika Jijini Arusha ambapo Mgeni Rasmi ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.