Dar es Salaam. Kuelekea kilele cha Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani, wanawake kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina wamewatembelea na kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa watoto wenye tatizo la saratani.
Watoto hao waliotembelewa siku ya Alhamisi, Machi 6, 2025, ni wale wa Kituo cha Tumaini la Maisha Tanzania, chenye makao makuu jijini Dar es Salaam.
Miongoni mwa mahitaji yaliyopelekwa ni pampasi, nazi kwaajili ya kutengenezea lishe, mashine ya kukandia ngano, sabuni za kuogea, mafuta ya kupaka, madaftari, vitabu vya hadithi, ‘ream papers’, na kalamu za risasi.
Mahitaji mengine ni kanga, feni, dawa za mbu, mifagio ya ndani, spika kubwa na redio ikiwa na kipaza sauti, pamoja na fedha taslimu.
Katika kituo cha Tumaini la Maisha, Dar es Salaam, kuna wagonjwa 22, wengi wao wakiwa ni watoto.
Kituoni hapo, kila mgonjwa anaishi na mwangalizi wake mmoja.
Kiongozi wa msafara wa watumishi waliotembelea kituo hicho, Bi Fatuma Mrope, ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Ofisi ya Msajili wa Hazina, alisema uamuzi wa kutoa msaada katika kituo hicho ulitokana na kuguswa na afya za watoto hao.
“Hawa ni watoto wetu hivyo tunajukumu la kuhakikisha tunakuwa sehemu ya kutengeneza tabasamu lao,” alisema Bi. Mrope, huku akiwaombea kwa Mwenyezi Mungu wapate uponyaji wa haraka.
Naye Bi. Linah Igogo, ambaye ni Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mfuko wa uwekezaji, Ofisi ya Msajili wa Hazina, alitoa rai kwa watanzania kuguswa na kuwasaidia watoto hao.
“Watoto hawa wanahitaji faraja yetu hivyo itakuwa vema kama tukiwashika mkono,” alisema Bi. Igogo.
Kwa upande wake, Bi. Neema Musomba, Mkurugenzi wa Huduma za Kimenejimenti kutoka Ofisi ya Msajili w Hazina, alionekana akizungumza lugha moja na Bi. Igogo.
“Tunapaswa kuwasaidia wenye uhitaji kwani kufanya hivyo ni ibada,” alisema Bi. Musomba.
Akipokea msaada, Bi. Elizabeth Chabiko, Afisa Msimamizi programu ya watoto katika kituo cha Tumaini la Maisha Tanzania, aliwashukuru wanawake kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa moyo wao wa upendo.
Alisema kituo hicho kina uhitaji mkubwa kwani gharama za uendeshaji ziko juu.
Bi. Chabiko alisema kituo hicho, kupitia fedha zinazotolewa na wasamaria wema, kinagharamia matibabu ya wagonjwa, pamoja na chakula na malazi kwa wagonjwa na waangalizi wao.
Pia, taasisi inasaidia kusomesha madaktari na manesi ambao baada ya kuhitimu masomo yao huanza kusaidiana kufanya kazi na wale wa serikali.
Alisema wagojwa wengi kutoka kituo cha Tumaini la Maisha Tanzania ni wale wa saratani ya; damu, jicho, figo, mifupa, matezi na ngozi.
Bi Asha Ally, mkazi wa Tanga, ambaye yupo katika kituo hicho cha Tumaini la Maisha kwa kipindi cha mwezi mmoja sasa, alisema bila msaada familia yake isingeweza kumudu gharama za matibabu kwani zipo juu sana.
Bi. Ally ambaye anauguza mdogo wake aitwaye Fatuma Ally, mwanafunzi wa kidato cha nne, alisema kidonge kimoja cha mionzi kina gharimu Sh2.7 milioni