Na Mwandishi wetu
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, ameitunuku Benki ya NMB cheti cha shukrani kwa mchango wake katika ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kahimba, wilayani Buhigwe, mkoani Kigoma.
Akipokea cheti hicho kwa niaba ya benki, Meneja wa NMB Kanda ya Magharibi, Restus Assenga, alieleza kuwa NMB itaendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha sekta ya elimu, hasa kwa wasichana, kama sehemu ya dhamira yake ya kuleta maendeleo endelevu katika jamii.
Sherehe hiyo pia ilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Kamishna Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto, Mhe. Thobias Andengenye, Meneja Mahusiano ya Benki na Serikali wa NMB Kanda ya Magharibi, Suma Mwainunu, Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Mhe. Kanali Michael Ngayalina, na Meneja wa NMB Tawi la Buhigwe, Pendo Waziri.
Mchango wa NMB katika mradi huu ni sehemu ya azma ya benki hiyo kusaidia maendeleo ya sekta ya elimu nchini kupitia uwekezaji wa rasilimali katika miundombinu ya shule ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunza.