Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Jacob Mkunda akikabidhi rambirambi kwa wazazi wa Private John Nyewata kwa niaba ya Rais Dkt.Samia Suluhu

…………..
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Jacob Mkunda amefika Jijini Mwanza kwaajili ya kuifariji familia ya Private John Nyewata aliepoteza maisha Januari 27 mwaka huu wakati alipokuwa akitekeleza majukumu yake ya kurejesha amani iliyopotea Mashariki mwa Congo.
Jenerali Mkunda amefika kwenye familia hiyo Leo Ijumaa Machi 07, 2025 kwaajili ya kuwapa mkono wa pole kwaniaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu.
Amesema Jeshi la wananchi la Tanzania linamajukumu ya msingi ikiwemo ulinzi wa amani,kusaidia nchi jirani ambazo amani imeteteleka.
Amesema kunavikundi vingi ambavyo viko nje ya nchi hii kwaajili ya kutekeleza suala la ulinzi, kunakikundi ambacho kiko Lebanoni ambayo iko inje ya Afrika, kunakikundi kipo Afrika ya kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na vingine viko Msumbiji.
“Kijana wetu alitumwa na Taifa kwenda kuwasaidia majirani zetu kurejesha amani walioipoteza lakini katika jitihada za kuitafuta amani hiyo alishambuliwa na kundi la waasi wa M23 Mashariki mwa Congo na mwili wake ulipumzishwa kwenye nyumba yake ya milele Februari 13 mwaka huu Mkoani Mara”, Amesema Jenerali Mkunda
Aidha, ameeleza kuwa Tanzania imekuwa na utaratibu wa kusaidia nchi za jirani tangu enzi za muasisi wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Kwa upande wake Baba Mzazi wa Private John Nyewata, Nyewata Kibwe amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwanamna anavyoendelea kuwafariji katika kipindi hiki cha majonzi.