Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mheshimiwa Dkt. Stergomena Tax (Mb), tarehe 05 Machi, 2025 amefanya ziara ya kikazi katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi kilichopo Monduli Jijini Arusha.
Ziara hiyo ya Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa katika chuo hicho cha mafunzo ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, aliambatana na kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa Ujenzi Jengo la kulala Askari Kapera wanawake wa chuo hicho unaotarajiwa kukamilika Novemba 2025.
Mara baada ya kufika katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli, Waziri Tax alipewa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa mradi huo unaoendelea na Mkuu wa Chuo hicho, Meja Jenerali Jackson Jairos Mwaseba, na kufahamishwa kuwa mradi huo wa ujenzi utachukua wiki 68 hadi kukamilika kwake Novemba 2025.
Akizungumza wakati wa kutembelea mradi huo na chuo hicho, Waziri wa Ulinzi na JKT ameupongeza Uongozi mzima wa chuo hicho kwa kuendelea kutoa mafunzo kwa maafisa wanafunzi wa Tanzania na nchi rafiki kwani mafunzo yanayotolewa chuoni hapo yana manufaa na maslahi mapana katika Ulinzi na usalama wa nchi na ustawi wa maendeleo kijamii na Amani na Utulivu wa nchi.
Waziri wa Ulinzi na JKT, Dkt Stergomena Tax akatumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuliwezesha Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Wizara kwa ujumla kiuwezo na kiutendaji katika miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo Ujenzi huo wa nyumba za kulala askari Kapera wanawake wa chuo.