Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze
Machi 6,2025
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, ambae pia ni Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, amekabidhi pikipiki 14, vishkwambi 15, na spika 15, vyenye thamani ya sh. mil 59,400,000 kwa maofisa maendeleo ya kata wa Halmashauri ya Chalinze.
Ameeleza vifaa hivyo vitasaidia kuboresha ufanisi wa kazi na kuwafikia wananchi kwa urahisi.
Aidha Ridhiwani alikabidhi hundi kwa vikundi ambapo anasema Halmashauri imetoa mikopo yenye thamani ya sh.milioni 721.022 kwa vikundi vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu.
“Fedha hiyo ni sehemu tu ya fedha iliyotengwa na halmashauri katika mwaka huu wa fedha kiasi cha sh. bilioni 2.2 kwa ajili ya kuwawezesha makundi hayo” alieleza Ridhiwani.
Alieleza fedha hizo sio zawadi, bali marejesho ndio faida yake ambapo mikopo ikirudishwa ndipo mzunguko unaendelea hivyo wakumbuke kurejesha.
Awali Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Nyamayao Said, alifafanua vifaa hivyo vitawasaidia maofisa maendeleo ya kata katika ufuatiliaji wa madawati sita ya maendeleo ya jamii, ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa mikopo, uhamasishaji wa uundaji wa vikundi, ufuatiliaji wa masuala ya ukatili wa kijinsia, na utoaji wa elimu kuhusu mambukizi ya UKIMWI na lishe.
Nae Ofisa Maendeleo, Ramadhani Abdala Mumba, alisema Halmashauri imeendelea kutekeleza kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kurejesha zoezi la utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu.
Hadi sasa, Halmashauri imetenga kiasi cha sh. bilioni 2.2 kati ya fedha hiyo imetoa sh.milioni 721.022 kwa vikundi vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu.
Mumba alieleza, kati ya hizo, milioni 316.016 imetolewa kwa vikundi vya wanawake, sh. milioni 371.006 kwa vikundi vya vijana, na sh.milioni 34 kwa vikundi vya watu wenye ulemavu.
Vilevile, aliongeza kusema, jumla ya vikundi 42 vimepatiwa mikopo, ambapo vikundi 41 ni vya wanawake, vikundi 16 ni vya vijana, na vikundi 5 ni vya watu wenye ulemavu.
“Idadi ya wanufaika wa moja kwa moja wa mikopo hiyo ni 324, ambapo wanawake ni 177 na wanaume ni 57”.
Mumba alifafanua, miradi ambayo imeidhinisha kupewa mikopo ni pamoja na kilimo, ufugaji, usafirishaji wa abiria (ikijumuisha boda boda na mabasi ya abiria), ujasiriamali wa maduka na bidhaa mbalimbali, maduka ya dawa muhimu, biashara ya fedha mtandao, na viwanda vidogo kama ushonaji wa nguo, viatu, na ufyatuaji wa matofali.
Akizungumzia changamoto, Mumba alieleza baadhi ya vikundi vimekosa ufanisi katika kutumia mfumo wa Wezesha Portal katika kuomba mikopo.
“Mtandao wa wezesha portal umeshindwa kuvuta taarifa za mfumo wa benki ili kudhibitisha akaunti za vikundi wakati wa kuomba mikopo” alifafanua Mumba.