Wanawake kutoka Wilaya mbalimbali za mkoa wa Mwanza wakiwa kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake katika uwanja wa Nyamagana

Mwalimu Sophia Turuya akisoma risala kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Mwanza kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake yaliyofanyika katika uwanja wa Nyamagana.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda akizungumza kwenye Maadhimisho ya siku ya wanawake
…….
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda ametaja mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika Sekta ya Afya ikiwemo kuongezeka kwa vituo vya Afya,Zahanati na Hospitali kutoka 321 mwaka 2021 hadi kufikia 549 mwaka 2025.
Mtanda ameeleza mafanikio hayo Leo Alhamis Machi 6, 2025 wakati akizungumza na wanawake,wananchi mbalimbali walioshiriki kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake ngazi ya mkoa yaliyofanyika katika uwanja wa mpira wa Nyamagana.
Mtanda amesema ongezeko hilo ni jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu za kuboresha sekta ya afya katika Mkoa wa Mwanza na Taifa kwaujumla.
Aidha, amesema mwaka 2021 hadi 2025 wataalamu wa afya 3,201 wameajiliwa hatua inayopelekea maendeleo ya sekta ya afya kuwa makubwa.
Amesema mwaka 2021 vifo vya akinamama wakati wa kujifungua vilikuwa 171 lakini kwa sasa ni 165 huku idadi ya vifo vya watoto ikipungua kutoka 859 mwaka 2021 hadi 700 kwa mwaka 2025.
“Sekta ya afya ni sekta nyeti na Serikali inaendelea kuboresha na kuongeza jitihada ili kuhakikisha vifo vya mama na mtoto vinaisha”, amesema Mtanda
Akisoma risala kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Mwanza, Mwalimu Sophia Turuya ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu kwakuboresha huduma za afya kwa hususani kwa wanawake na watoto.
“licha ya kuwepo kwa upungufu wa wataalamu wa afya hususani katika maeneo ya visiwa vilivyopo katika mkoa wa Mwanza tunaishukuru Serikari sana kwanamna inavyoendelea kuboresha sekta ya afya”, Amesema
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Christopher Ngubiagai amewataja wanawake wa ukerewe kuwa vinara na shupavu katika kujali na kubeba familia zao huku akitoa rai kwa wanaume kushikamana vyema na wake zao hatua itakayosaidia kupunguza matukio ya kikatili kwenye jamii.
Kauli mbiu ya Maadhimisho hayo ni ‘wanawake na wasichana 2025, tuimarishe haki,usawa na uwezeshaji’